Monday, February 3, 2014

MSHABIKI MBARONI KWA MADAI YA TIKETI FEKI.

MSHABIKI mmoja anashikiliwa na Jeshi la Polisi akidaiwa kukutwa na tiketi bandia kwenye mechi ya Ligi Kuu ya Vodacom (VPL) kati ya Yanga na Mbeya City iliyochezwa jana (Februari 2 mwaka huu) Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam. Matei Cosmas (28) ambaye ni mkazi wa Buza Njiapanda Kitunda, Dar es Salaam amefunguliwa jalada namba CHA/IR/900/2014 kwenye Kituo cha Polisi Chang’ombe akidaiwa kupatikana na tiketi bandia. Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) leo asubuhi (Februari 3 mwaka huu) limeamkia Kituo cha Polisi Chang’ombe kusaini hati ya maelezo dhidi ya mtuhumiwa. Ni imani ya Shirikisho kuwa mtuhumiwa atachukuliwa hatua kwa mujibu wa sheria za nchini. Tunatoa mwito kwa washabiki wa mpira wa miguu kuepuka kununua tiketi kutoka mikononi mwa watu, kwani kufanya hivyo ni kosa. Tiketi zinauzwa kwenye sehemu maalumu zenye chapa ya TFF.



RAIS WA TFF ATEMBELEA RUANGWA
Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Jamal Malinzi ametembelea Chama cha Mpira wa Miguu Wilaya ya Ruangwa mkoani Lindi. Katika ziara hiyo aliyoifanya jana (Februari 2 mwaka huu), pia alikuwa mgeni rasmi mechi ya kugombea Kombe la Majaliwa kati ya Hull City na Mbagala City, na kuahidi kuwa TFF itaandaa kozi za awali za ukocha na uamuzi kwa Wilaya ya Ruangwa.

No comments:

Post a Comment