BEKI wa zamani wa Barcelona, Miguel Angel Nadal amesema Neymar anaonewa kutokana na matatizo ya hivi karibuni ya klabu hiyo na anaamini kuwa hapaswi kuhusishwa. Uchunguzi juu ya uhamisho wa mshambuliaji huyo katika majira ya kiangazi kutoka klabu ya Santos umepelekea aliyekuwa rais wa Barcelona Sandro Rossell kujiuzulu mwezi uliopita na nafasi yake kuchukuliwa na Josep Maria Bartomeu ambaye alianza kwa kuwataja waliohusika na usajili huo. Matokeo yalionyesha kuwa Barcelona ilitumia jumla ya euro milioni 86.2 katika usajili wa nyota huyo, ingawa wenyewe walidai kutumia euro milioni 57.1 pekee. Pia ilibainika kuwa Barcelona walilipa ada ya euro milioni 40 kwa wazazi wa nyota huyo na sasa Bartomeu anakabiliwa na kesi mbili nchini Hispania na Brazil. Nadal ambaye ni mjomba wa nyota wa tenisi Rafael Nadal amesema Neymar bado ni mdogo sana na hawezi kuwa alihusika na masuala hayo yote. Nadal ameendelea kudai kuwa mchezaji huyo hatakiwi kuhusishwa na chochote kuhusu hilo kwani kitu pekee alichofanya yeye ni kwenda Barcelona kwakuwa walimhitaji.
No comments:
Post a Comment