MICHUANO ya Ligi ya Mabingwa barani Ulaya itaendelea kutimua vumbi tena leo na kesho katika hatua ya mtoano ya timu 16 bora kwa vilabu kuonyeshana kazi katika viwanja mbalimbali. Toka kubadilishwa jina kwa michuano hiyo na kuitwa Ligi ya Mabingwa miaka 22 iliyopita hakuna klabu yoyote barani humo iliyowahi kutetea taji lake huku AC Milan ikiwa klabu pekee iliyowahi kufanya hivyo katika miaka ya 1990 wakati huo michuano hiyo ikiitwa Kombe la Ulaya au European Cup. Wiki hii viwanja vinne vinatarajiwa kuwaka moto kwenye mechi za mkondo wa kwanza ambapo katika mechi za leo usiku macho na masikio ya mashabiki yako katika mchezo utakaowakutanisha wenyeji Manchester City na Barcelona katika Uwanja wa Etihad huku mchezo mwingine ukiwa kati ya Bayer Liverkusen na matajiri wa Ufaransa timu ya Paris Saint-Germain, PSG. Mabingwa watetezi wa michuano hiyo Bayern Munich ya Ujerumani wao Jumatano watakuwa na kibarua cha kujaribu kuwa timu ya kwanza kunyakuwa taji hilo kwa mara ya pili pale watakapokuwa wageni wa Arsenal katika Uwanja wa Emirates wakati AC Milan wao wataikaribisha Atletico Madrid katika Uwanja wa San Siro.
No comments:
Post a Comment