Tuesday, February 18, 2014

MICHUANO YA KOMBE LA DUNIA BRAZIL ITAKUWA NA MAFANIKIO - HODGSON.

KOCHA wa timu ya taifa ya Uingereza, Roy Hodgson amesema ana uhakika Brazil itaandaa michuano ya Kombe la Dunia yenye mafanikio pamoja na matatizo ya viwanja na maandamano. Hodgson yuko katika ziara huko Manaus ambako Uingereza itakabiliana na Italia katika mchezo wa ufunguzi katika uwanja wa Amazonia lakini kumekuwa na wasiwasi kuwa uwanja huo ambao bado haujamalizika unaweza kuondolewa katika orodha ya viwanja vitakavyotumika kwa ajili ya michuano hiyo. Hodgson amesema Shirikisho la Soka Duniani, FIFA na serikali ya Brazil wamefanya kazi kubwa hivyo haoni sababu kwa watu kutilia shaka maandalizi ya michuano hiyo. Kumekuwa pia na wasiwasi wa kurudia kwa maandamano kama ilivyokuwa katika michuano ya Kombe la Shirikisho lakini kocha huyo amedai kuwa ana imani na kamati ya maandalizi itafanya kazi ipasavyo. Michuano hiyo inatarajiwa kuanza nchini humo Juni 12 mwaka huu lakini Uwanja wa Sao Paulo ambao utatumika kwa ajili ya mechi ya ufunguzi bado unaonekana kuwa katika matengenezo. Viwanja vitano vitakavyotumika katika michuano hiyo vimeshindwa kuwa tayari katika muda wa mwisho uliopangwa na FIFA ambao ni Desemba 31 mwaka jana lakini katibu mkuu wa shirikisho hilo Jerome Valcke amebainisha kuwa amefurahishwa na maendeleo yake kwani vimekamilika kwa asilimia 97.

No comments:

Post a Comment