Saturday, April 26, 2014

ULIMWENGU WA SOKA WAOMBOLEZA KIFO CHA TITO VILANOVA.

ULIMWENGU wa soka mwishoni mwa wiki hii umeamka na majonzi makubwa kufuatia kifo cha meneja wa zamani wa Barcelona Tito Vilanova kilichotokea jana. Vilanova amekuwa akipambana na maradhi ya saratani lakini taarifa za kifo chake zimeonyesha kumshitua na ghafla kwa kila mtu wakiwemo nyota wengi wa Barcelona. Rais wa klabu hiyo Josep Maria Bartomeu katika salamu zake za rambirambi amemuelezea Vilanova kama mkufunzi ambaye ameondoka lakini hawezi kusahaulika kamwe kutokana na ushujaa wake. Salamu zingine za rambirambi zimeendelea kumiminika kutoka kwa wachezaji wa Barcelona akiwemo Andres Iniesta, Xavi, Lionel Messi, Cesc Fabregas na wengineo. Katika salamu wengi wao wameonyesha kukumbuka mengi aliyoyafanya kocha huyo toka akiwa mwalimu katika shule ya soka ya Barcelona iitwayo La Masia mpaka alipopanda na kuwa kocha mkuu. Vilanova amefariki dunia akiwa na umri wa miaka 45, na kuacha watoto wawili na mke baada ya kushindwa mapambano na saratani ya koo aliyopata toka mwaka 2011.


No comments:

Post a Comment