ADHABU HAITATUZUIA KUFANYA USAJILI TUNAOTAKA - AL MUBARAK
MWENYEKITI wa klabu ya Manchester City, Khaldoom Al Mubarak amesema mabingwa hao wa Ligi Kuu nchini Uingereza watafanya usajili wa haraka pamoja na adhabu waliyopewa na Shirikisho la Soka la Ulaya-UEFA. City wametozwa faini ya paundi milioni 49, na kuruhusiwa kutumia wachezaji 21 katika michuano ya Ligi ya Mabingwa barani Ulaya baada ya kushindwa kutimiza masharti ya sheria ya matumizi ya fedha. Adhabu nyingine inamaanisha City wataruhusiwa kutumia kiasi cha paundi milioni 49 pekee katika usajili kiangazi hiki pamoja na ada yoyote watakayopata kwa ajili ya kuuza mchezaji. Al-Mubarak amesema wanajua aina ya wachezaji wanaotakiwa kuondoka na wanaotakiwa kununuliwa ikiwemo maeneo ambayo yanatakiwa kuboreshwa hivyo amewaondoa hofu mashabiki wa timu hiyo. City walitawadhwa mabingwa wapya wa ligi kwa mara ya pili kwenye kipindi cha miaka mitatu baada ya kumaliza kwa tofauti ya alama mbili na Liverpool walioshika nafasi ya pili.
No comments:
Post a Comment