KOCHA wa timu ya taifa ya Hispania, Vicente del Bosque anategemea Diego Costa atapona kwa wakati kutokana na majeraha ya msuli yanayomsumbua lakini anaamini mabingwa hao wa Ulaya na Dunia wanao wachezaji wengi wanaoweza kuziba nafasi yake kama akishindwa. Mshambuliaji huyo wa Atletico Madriod amekuwa akisumbuliwa na majeruhi ya msuli kwa takribani wiki mbili na kulazimika kutolewa nje katika dakika ya tisa ya mchezo wa fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya dhidi ya Real Madrid iliyochezwa Jumamosi iliyopita. Del Bosque amesema nyota huyo ana majeruhi ya msuli ambayo watakuwa wakiyatizama maendeleo yake ili waweze kufanya uamuzi katika dakika za mwisho. Kocha huyo aliendelea kudai kuwa bado wana nafasi mpaka Juni 2 ili waweze kutaja kikosi chao cha mwisho cha wachezaji 23 hivyo haoni haja ya kuwa na haraka, kwani ikishindikana bado wanao wachezaji wengine wazuri wanaoweza kuziba nafasi yake. Kama nyota huyo mzaliwa wa Brazil akishindwa kupona kwa wakati kwa ajili ya michuano hiyo, Del Bosque bado ana wachezaji kama Fernando Torres, Alvaro Negredo na Fernando Llorente ambao wanaweza kuziba nafasi hiyo vyema. Hispania itacheza mechi yake ya kujipima nguvu dhidi ya Bolivia jijini Seville, Ijumaa hii baada ya wachezaji wa Atletico na Real Madrid waliocheza katika fainali kujiunga na kikosi cha nchi hiyo.
No comments:
Post a Comment