KLABU ya Bayern Munich imedai kumuongeza mkataba mshambuliaji wake, Claudio Pizarro kwa msimu mmoja zaidi utakaomalizika mwakani. Nyota huyo wa kimataifa wa Peru mwenye umri wa miaka 35 alijiunga na Bayern mwaka 2012 kwa mara ya pili baada ya kuichezea Werder Bremen kwa miaka mitatu na kufunga mabao 10 katika mechi 17 alizocheza msimu uliopita ambapo mara nyingi alikuwa akianzia benchi. Pizarro ambaye anaongoza wachezaji wa kigeni kwa kufunga mabao mengi katika Bundesliga akiwa amefunga mabao 176 katika mechi 370 alionekana chaguo sahihi kwa Pep Guardiola baada ya mshambuliaji nyota wa kutegemewa Mario Mandzukic aliposhindwa kuelewana na kocha huyo mwishoni mwa msimu. Katika taarifa yake Ofisa Mkuu wa Bayern Karl-Heinz Rummenigge amesema Pizarro ameonyesha msimu huu jinsi gani alivyokuwa hatari anapokuwa karibu lango la wapinzani na jinsi gani alivyo muhimu katika timu. Rummenigge amesema anafurahi kwamba wataendelea kupata huduma ya mchezaji huyo kwa msimu mwingine. Pizarro alicheza bayermn kuanzia mwaka 2001 hadi 2007 kabla ya kurejea Bremen mwaka 2009 ambako aliwahi kucheza kuanzia mwaka 1999-2001, baada ya misimu miwili yenye mafanikio katika klabu ya Chelsea.
No comments:
Post a Comment