MSHAMBULIAJI nyota wa klabu ya Liverpool Luis Suarez ameongeza tuzo katika orodha yake ya tuzo zake, baada ya kuteuliwa kuwa mchezaji bora wa Ligi Kuu ya Uingereza msimu wa 2013-2014. Nyota huyo amefunga mabao 31 na kutoa pasi 12 za mabao katika mechi 33 za ligi alizocheza, huku timu yake Liverpool ikizidiwa kidogo na Manchester City katika mbio za ubingwa. Suarez, ambaye pia ameshinda tuzo ya Mchezaji Bora wa Wachezaji wa PFA na Mchezaji Bora wa Waandishi wa habari za Soka msimu huu, ameshinda tuzo ya nne msimu huu pamoja na ile ya kiatu cha dhahabu. Tuzo hiyo Suarez imekuja ikiwa ni saa chache baada ya meneja wa Liverpool Brandan Rodgers naye kutunukiwa tuzo ya kocha bora wa mwaka na Chama cha Makocha wa Ligi nchini humo. Rodgers amekuwa na msimu mzuri akiiongoza timu hiyo ya Merseyside kumaliza nafasi ya pili kwenye ligi. Kocha wa timu ya taifa ya Uingereza, Roy Hodgson ndiye alimkabidhi tuzo hiyo kocha huyo mwenye umri wa miaka 41, ambayo hutokana na kura zinazopigwa na makocha kutoka timu za madaraja yote manne.
No comments:
Post a Comment