Thursday, June 12, 2014

ARSENAL YAANZA USAJILI KWA MAKEKE, YAANZA NA KOCHA MPYA WA VIUNGO ILI KUKABILIANA NA MAJERUHI.

KLABU ya Arsenal imepiga hatua kubwa ili kupunguza balaa la majeruhi linalowasumbua mara kwa mara kwa kuajiri mwalimu mpya wa viungo. Shad Forsythe ambaye ni kocha mkuu wa viungo wa timu ya taifa ya Ujerumani amefikia makubaliano ya kujiunga na benchi la ufundi la Arsene Wenger baada ya michuano ya Kombe la Dunia. Forsythe mwenye umri wa miaka 40 raia wa Marekani anatarajia kufanya kazi sambamba na Tony Colbert ambaye amekuwa kocha wa viungo katika kikosi cha kwanza cha Arsenal kwa kipindi cha miaka 16, ikiwa ni sehemu ya mikakati ya Wenger kukomesha tatizo la majeruhi ambalo limekuwa likiiyumbisha timu yake kwa miaka kadhaa. Wenger aliapa kuangalia upys mazoezi na matibabu wanayopatiwa wachezaji wake kufuatia kupatwa na balaa hilo la majeruhi katika mzunguko wa pili wa ligi msimu huu na kuwakosa nyota wake wengi kama Aaron Ramsey, Mesut Ozil, Theo Walcott na Jack Wilshere. Kwa mujibu wa uchunguzi uliofanywa na mtandao wa physioroom.com, wachezaji wa Arsenal inasemakana walikosekana kwa siku nyingi zaidi msimu uliopita kutokana na majeruhi kuliko klabu yoyote katika Ligi Kuu. Forsythe aliteuliwa mwaka 2004 kuwa mwalimu wa viungo wa timu ya taifa ya Ujerumani na meneja wa zamani wa timu hiyo Jurgen Klinsmann na katika kipindi cha miaka 10 amekuwa akifanya shughuli hiyo.

No comments:

Post a Comment