MWANAMUZIKI nyota wa muziki wa Pop kutoka Marekani, Jennifer Lopez maarufu kwa jina la J-Lo anatarajiwa kupamba sherehe za ufunguzi wa michuano ya Kombe la Dunia kwa kuimba wimbo maalumu wa We are One. Wimbo huo ambao ni maalumu kwa ajili ya michuano hiyo, J-Lo ataimba sambamba na rapa Pitbull pamoja na mwanamuziki mahiri wa Brazil Claudia Leitte. Awali kulikuwa na mashaka ya kutokuwepo kwa J-Lo baada ya Jumapili iliyopita Shirikisho la Soka Duniani-FIFA kutangaza kuwa mwanamuziki huyo alikuwa amejitoa kutokana na masuala ya production lakini baadae walibatilisha taarifa hiyo na kudai atakuwepo katika ufunguzi ingawa hawakutoa sababu zilizomfanya abadili mawazo. Ingawa wimbo huo mpaka sasa umetizamwa na watu zaidi milioni 75 katika mtandao wa You Tube baadhi ya watu wameuponda na kudai haujazidi ule wa Rick Martin wa Cup of Life alioimba katika michuano hiyo mwaka 1998 na ule wa Waka Waka alioimba Shakira katika michuano iliyopita iliyofanyika Afrika Kusini. Mashabiki zaidi ya 60,000 wanatarajiwa kuwepo katika Uwanja wa Corinthians leo wakiwemo viongozi wa 12 kutoka nchi mbalimbali na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon huku watu zaidi ya bilioni moja duniani kote wakitarajiwa kushuhudia sherehe hizo kupitia katika luninga zao.

No comments:
Post a Comment