KLABU ya Barcelona, imemfungulia milango kiungo wake mahiri Xavi na kumpasha kuwa anaweza kuondoka kiangazi hiki kama atahitaji kufanya hivyo. Kocha wa klabu ya Al-Arabi, Dan Petrescu amedai jana kuwa kiungo huyo amesaini mkataba wa awali wa makubaliano na timu hiyo ya Qatar, ingawa mwenyewe bado hajatoa uamuzi wa mwisho kuhusiana na mustakabali wake. Xavi kwasasa yuko nchini Brazil kwenye michuano ya Kombe la Dunia na timu yake ya taifa ya Hispania, lakini wakala wake Ivan Corretja amekutana na rais wa Barcelona Josep Maria Bartomeu na mkurugenzi wa michezo Andoni Zubizarreta kuzungumzia masuala ya mchezaji huyo jana. Hata hivyo hakuna uamuzi wowote uliofikiwa katika mkutano huo na kocha wa timu hiyo Luis Enrique ameweka nia ya kukutana na kiungo huyo moja kwa moja ili kuzungumzia mipango ya msimu ujao. Kiungo huyo ambaye alikaribia kujiunga na klabu za Manchester United na Bayern Munich wakati anaanza soka kulipwa, amecheza mechi 700 za mashindano akiwa na Barcelona na kushinda mataji 22.
No comments:
Post a Comment