KIUNGO wa zamani wa Kimataifa wa Uingereza, Paul Scholes amemsisitiza kocha wa timu ya taifa ya nchi hiyo Roy Hodgson kutumia mbinu za Sir Alex Ferguson ili kuweza kumzuia Andrea Pirlo wakati watakapokutana na Italia Juni 14 katika michuano ya Kombe la Dunia. Scholes aliandika hayo katika blog yake ya Paddy Power na kudai kuwa Muitaliano huyo ndio kiungo mchezeshaji bora kabisa duniani. Lakini anaamini United ilionyesha jinsi gani ya kumzuia wakati Ferguson alipomkabidhi Park Ji-Sung majukumu ya kumzuia kiungo huyo wakati walipokutana na AC Milan katika michuano ya Ligi ya Mabingwa barani Ulaya mwaka 2010. Scholes aliandika kuwa Pirlo ni kiungo bora na aliyekamilika na kama ukimpa muda na nafasi hakuna shaka kwamba lazima akusambaratishe na ili uweze kumzuia unatakiwa kumnyima hivyo viwili. Kiungo huyo anamkumbuka Pirlo alivyowahenyesha wakati Uingereza ilipotolewa na Italia katika michuano ya Ulaya mwaka 2012. Scholes amesema ingawa mechi iliisha kwa sare ya bila ya kufungana lakini anakumbuka Pirlo alikimbia kilomita 11.58 kuliko mchezaji yoyote wa Uingereza kwenye mechi hiyo huku akitoa pasi zaidi ya 131.

No comments:
Post a Comment