MSHAMBULIAJI wa kimataifa wa Uruguay na klabu ya Liverpool Luis Suarez ameibuka na kumuomba radhi beki wa Italia Giorgio Chiellini kufuatia tukio la kumng’ata wakat timu zilipokutana katika mechi za mwisho za makundi katika michuano ya Kombe la Dunia inayoendelea nchini Brazil. Suarez alitumia ukurasa wake wa mtandao wa kijamii wa twitter kuomba radhi kutokana na tukio hilo baada ya kutulia nyumbani na familia yake na kugundua kuwa hakufanya kitendo cha uungwana na hatarudia tena. Nyota huyo aliendelea kuandika kuwa anajutia sana tukio hilo na anamuomba radhi Chiellini huku akikiri kutorudia tena kitendo hicho. Shirikisho la Soka Duniani-FIFA lilimpa adhabu Suarez ya kutojishughulisha na mambo yoyote yahusuyo mchezo wa soka kwa muda wa miezi minne sambamba na kumfungia mechi tisa za kimataifa pamoja na faini ya paundi 65,000. Katibu mkuu wa FiFa Jerome Valcke alimtaka Suarez atafute matibabu ya kisaikolojia wakati akitumikia adhabu hiyo ili asiweze kurudia tena kitendo hicho ambacho amekifanya zaidi ya mara mbili kwa nyakati tofauti.
No comments:
Post a Comment