WASHAMBULIAJI Mbwana Samata na Thomas Ulimwengu wamewasili nchini leo asubuhi wakitokea nchini Tunisia ili kujiunga na Taifa Stars kwa ajili ya mechi dhidi ya Msumbiji itakayochezwa Jumapili kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam. Wachezaji hao wamefikia hoteli ya Courtyard, Seaview Upanga na wanatarajiwa kufanya mazoezi kwa programu maalumu waliyopewa na kocha mkuu wa Taifa Stars, Mart Nooij wakati wakiwasubiri wenzao waliopo Mbeya. Mbali na hao pia kiungo Mwinyi Kazimoto anayecheza soka la kulipwa katika katika klabu ya Almarhiya ya Qatar atawasili nchini kesho asubuhi kwa ndege ya Qatar ili kuiongezea nguvu Stars. Kikosi kamili cha Stars nacho kinatarajiwa kutua jijini Dar es Salaam kesho wakitokea katika kambi yao waliyoweka jijini Mbeya tayari kwa ajili ya maandalizi ya mwisho ya kuivaa msumbiji. Wakati huohuo kuna taarifa kuwa tayari kikosi cha timu ya taifa ya Afrika Kusini kimewasili jijini Dar es Salaam kwa ajili ya mchezo dhidi ya timu ya taifa ya Tanzania-Serengeti Boys. Mchezo huo utakuwa wa mkondo wa kwanza wa mzunguko wa pili wa michuano ya Afrika kwa vijana wenye umri chini ya miaka 17 utakaochezwa Ijumaa Julai 18 katika Uwanja wa Azam Complex,Mbagala jijini Dar es Salaam.

No comments:
Post a Comment