SHIRIKISHO la Soka nchini-TFF, limekiri kukamatwa kwa basi lake na madalali kwa amri ya mahakama kutokana na deni la shilingi milioni 140 wanazodaiwa. Kwa mujibu wa taarifa iliyotumwa na Ofisa habari wa TFF, Boniface Wambura imedai kuwa amri hiyo imetokana na deni hilo la kampuni ya Punchline ya Kenya iliyokuwa ikichapa tiketi za kuingilia uwanjani kuanzia mwaka 2007. Hadi sasa shirikisho hilo limelipa kiasi cha shilingi milioni 70 katika deni hilo. Taarifa hizo zinakanganyana na zile zilizotolewa jana Katibu Mkuu wa TFF, Selestine Mwesigwa ambaye alikanusha kukamatwa kwa mali za shirikisho hilo ingawa akiliri kuwepo kwa deni hilo. Mwesigwa alidai kuwa deni hilo lilikuwa la mwaka 2010 na lilitokana na uchapishaji wa tiketi na kwamba walishalipa kiasi cha shilingi milioni 50 na kubaki deni la milioni 90.
No comments:
Post a Comment