Wednesday, September 24, 2014

KOCHA WA ELCHE AMFANANISHA RONALDO NA MICHAEL JORDAN BAADA YA KUTUPIA NNE.

MENEJA wa klabu ya Elche, Fran Escriba amemfananisha Cristiano Ronaldo na nguli wa mpira wa kikapu nchini Marekani Michael Jordan baada ya mshambuliaji huyo wa Real Madrid kuonyesha kiwango cha hali ya juu katika mchezo wa La Liga uliochezwa jana. Katika mchezo huo Ronaldo alifunga mabao manne wakati Madrid walipotoka nyuma na kuibuka na ushindi wa mabao 5-1 katika Uwanja wa Santiago Bernabeu. Ronaldo mwenye umri wa miaka 29 sasa ameipita rekodi ya Santillana kwa kuwa mfungaji wa tatu aliyefunga mabao mengi zaidi katika klabu hiyo kwa kufikisha mabao 187 huku akifunga hat-trick yake ya 25 akiwa na Madrid toka alipotoka Manchester United mwaka 2009. Sasa Ronaldo anakaribia rekodi iliyowekwa na nguli Alfredo Di Stefano ambaye ndio kinara wa mabao anayeoongoza katika klabu hiyo kwa kipindi chote. Escriba alimmwagia sifa Ronaldo baada ya mchezo huo kwa kumfananisha na Jordan ambaye amewahi kushinda mataji sita ya Ligi ya Mpira wa Kipapu nchini Marekani-NBA huku akinyakuwa tuzo tano za mchezaji mwenye thamani zaidi-MVP. Escriba amesema Ronaldo ni mchezaji wa kipekee mwenye uwezo wa hali ya juu kufunga ndio maana anamfananisha na Jordan enzi zake wakati akicheza na kufunga alama 50 katika mechi moja.

No comments:

Post a Comment