MENEJA mpya wa klabu ya Schalke, Roberto Di Matteo anatarajiwa kuanza kibarua chake cha kuipandisha timu hiyo katika msimamo wa Bundesliga Jumamosi hii wakati atakapokwaana na Hertha Berlin wakati mahasimu wao Borussia Dortmund wao watakuwa wakihitaji ushindi katika mchezo wao dhidi ya Cologne. Schalke kwasasa inashika nafasi ya 11 katika msimamo wa ligi na inategemewa Di Matteo ataleta matumani mapya baada ya kutimuliwa kwa meneja Jens Keller kufuatia kipigo cha mabao 2-1 dhidi ya Hoffenheim. Golikipa wa Schalke Ralf Faehrmann amesema Di Matteo anafanya kazi nzuri kwani wanafanya mazoezi kwa wingi hivyo kukosa nafasi ya kufikiria yaliyotokea. Kama ilivyokuwa kwa timu zingine katika ligi hiyo nafasi ya Schalke kufanya mazoezi ya pamoja ilikwamishwa na mapumziko ya mechi za kimataifa lakini golikipa huyo bado ana matumaini katika siku hizi chache zilizobakia wataweza kuijiandaa vya kutosha kwa ajili ya mchezo wao huo. kwa upande wa Dortmund ambao wanashika nafasi ya 13 katika msimamo wa ligi hivi, watapumua kidogo baada ya baadhi ya wachezaji wake majeruhi kuanza kurejea akiwemo mshambuliaji Marco Reus na kiungo Henrikh Mkhitaryan wakitegemewa kuwepo katika mchezo dhidi ya Cologne. Kwa upande mwingine vinara wa ligi hiyo Bayern Munich wao watakuwa wenyeji wa Werder Bremen ambao wanashika mkia kwasasa katika msimamo mchezo ambao winga Franck Ribery anaweza kurejea kutoka katika majaruhi yaliyokuwa yakimsumbua.

No comments:
Post a Comment