MENEJA wa klabu ya Arsenal, Arsene Wenger amethibitisha leo kuwa atamkosa kiungo wake majeruhi Aaron Ramsey kwa muda wa wiki nne au zaidi. Nyota huyo wa kimataifa wa Wales alipata majeruhi ya msuli wa nyuma ya paja wakati wa mchezo wa Ligi Kuu uliokwisha kwa sare ya bao 1-1 dhidi ya Tottenham Hotspurs Jumamosi iliyopita hatua mbayo ilimfanya kukosa mchezo wa Ligi ya Mabingwa Ulaya Jumatano. Vyombo vya habari nchini Uingereza vimeripoti leo kuwa Ramsey anaweza kuwa nje ya uwanja kwa zaidi ya miezi minne lakini Wenger amesema nadhani kiungo huyo mwenye umri wa miaka 23 anaweza kurejea uwanjani mwanzoni mwa mwezi ujao. Wenger amesema kwa mujibu wa madaktari Ramsey anaweza kuwa nje kwa muda wa wiki tatu mpaka nne hivyo yeye ameamua kuhesabu nne kabisa. Kama nyota huyo akikaa nje kwa muda huo ataikosa michezo ya Ligi Kuu dhidi ya Chelsea, hull City na Sunderland pamoja na mchezo wa ugenini wa Ligi ya Mabingwa Ulaya dhidi ya Anderlecht.

No comments:
Post a Comment