KIUNGO wa kimataifa wa Ghana na klabu ya Juventus, Kwadwo Asamoah anatarajiwa kuwa nje ya uwanja kwa kipindi cha miezi mitatu baada ya kufanyiwa upasuaji jana hivyo kumfanya kukosa michuano ya Mataifa ya Afrika itakayofanyika mapema mwakani. Kwa mujibu wa taarifa wa klabu hiyo ambao ndio vinara na mabingwa watetezi wa Serie A, imedai kuwa upasuaji kwa Asamoah lilikuwa jambo la lazima na kupona kwake kunatarajiwa kuwa sio chini ya miezi mitatu. Asamoah mwenye umri wa miaka 25 ambaye hucheza nafasi ya kiungo wa kushoto na pia beki wa kushoto, katika kipindi cha miaka mitano amekuwa mchezaji muhimu katika kikosi cha Ghana na alicheza katika michuano ya Kombe al Dunia. Ghana ni mojawapo wa timu zinazopewa kipaumbele kunyakuwa michuano hiyo ya Afrika ambayo inatarajiwa kufanyika huko Guinea ya Ikweta kuanzia Januari hadi Februari mwakani. Mbali na Asamoah, Juventus pia imepata pigo lingine kwa kiungo wake mzaliwa wa Brazil Romulo naye kufanyiwa upasuaji kutokana na majeraha ya msuli yanayomsumbua huko Sao Paulo.
No comments:
Post a Comment