Friday, January 2, 2015

AFCON 2015: MALI KUMKOSA DIABATE.

MSHAMBULIAJI wa klabu ya Bordeaux ya Ufaransa, Cheick Diabate anatarajiwa kufanyiwa upasuaji wa goti ambao utamfanya kushindwa kujiunga na kikosi cha timu ya taifa ya Mali kwa ajili ya michuano ya Mataifa ya Afrika. Diabate ambaye ndio anaongoza akiwa ameufunga mabao nane katika klabu yake msimu huu, wiki iliyopita alitajwa katika kikosi cha mwisho cha wachezaji 23 wa Mali kwa ajili ya michuano hiyo itakayofanyika huko Guinea ya Ikweta. Bordeaux ilitangaza jana kuwa nyota huyo mwenye umri wa miaka 26 alikubali kufanyiwa upasuaji huo baada ya kushauriwa na mtalaamu jijini Marseille mwezi uliopita. Taarifa hiyo itakuwa pigo kubwa kwa kocha wa Mali Henryk Kasperczak kwani alikuwa akimtegemea mshambuliaji huyo kwa ajili ya michuano hiyo ya mwaka huu. Mali ambao katika michuano iliyopita walimaliza katika nafasi ya tatu, wamepangwa katika kundi gumu la D wakiwa sambamba na timu za Ivory Coast, Cameroon na Guinea.

No comments:

Post a Comment