MENEJA wa klabu ya Inter Milan Roberto Mancini amesisitiza anapaswa kubebeshwa lawama zote kwa kikosi chake kutolewa katika michuano ya Europa League na Wolfsburg ya Ujerumani jana. Inter walitakiwa kubadili matokeo ya kufungwa mabao 3-1 katika mchezo wao wa mkondo wa kwanza uliochezwa huko Volkswagen Arena lakini walishindwa kufanya hivyo na kujikuta wakichapwa mabao 2-1. Kocha huyo wa zamani wa Manchester City amekiri udhaifu katika safu yake ya ulinzi na kudai kuwa kama wanataka kurejea katika kiwango chao cha juu wanapaswa kufanyia kazi suala hilo. Mancini amesema waliufanya mchezo huo kuwa mgumu baada ya kukubali kufungwa mapema jambo lilifanya kila mpango waliojiwekea kubadilika. Hata hivyo kocha huyo aliendelea kudai kuwa walijitahidi kutengeneza nafasi nyingi za kufunga baada ya kuwa nyuma lakini bado mambo yaliwawia vigumu. Inter ambao sasa wanafikisha mechi yao ya tano bila ushindi wanakabiliwa na kibarua kingine Jumapili hii wakati watakapochuana na Sampdoria katika mchezo wa Serie A.
No comments:
Post a Comment