MSHAMBULIAJI nyota wa Paris Saint-Germain-PSG, Edinson Cavani amesisitiza hana mpango wa kuondoka katika klabu hiyo mwishoni mwa msimu huu. Nyota huyo wa kimataifa wa Uuruguay mara nyingi amekuwa akicheza kama winga toka atue Ufaransa akitokea Napoli katika majira ya kiangazi mwaka 2013 na amekuwa akihangaika kurejea katika kiwango chake. Katika mchezo wa jana Cavani alicheza katika nafasi aliyozoea ya mshambuliaji wa kati kutokana na Zlatan Ibrahimovic kutumikia adhabu yake lakini hata hivyo alishindwa kung’ara. Nyota huyo alikosa nafasi kadhaa za kufunga wakati PSG walipochapwa mabao 3-1 na Barcelona katika mchezo wa mkondo wa kwanza wa robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya huku akionekana kukosa hali ya kujiamini. Cavani amekuwa akihusishwa na tetesi za kutimkia Juventus na baadhi ya vilabu vya Ligi Kuu lakini mwenyewe amekanusha akidai kuwa bado anataka kuendelea kutumikia PSG kwani anauheshimu mkataba wake.
No comments:
Post a Comment