KLABU ya Chelsea imeanza mazungumzo na Atletico Madrid juu ya uwezekano wa kumsajili kiungo wao wa kimataifa wa Hispania Koke kwa kitita cha paundi milioni 30. Meneja wa Chelsea Jose Mourinho ambaye amenyakuwa taji la Ligi Kuu Jumapili iliyopita, tayari ameshaanza mipango ya kujiandaa na msimu ujao. Kuna nafasi kadhaa katika kikosi cha Chelsea ambazo Mourinho aanataka kuziongezea nguvu na nafasi ya kiungo ni mojawapo ndio maana amemuweka Koke katika orodha zake za juu za wachezaji anaotaka kuwasajili. Koke ana thamani ya paundi milioni 44 katika mkataba wake mpya wa miaka mitano aliosaini mwaka jana lakini Chelsea wanatarajia kumruhusu beki wa zamani wa Atletico Filipe Luis ambaye amshindwa kung’aa toka ajiunge nao kurudi Hispania hivyo kumaanisha wanaweza kulipa paundi milioni 30. Mkurugenzi wa ufundi wa Chelsea Michael Emenalo alisafiri kwenda Hispania kumtizama Koke wiki iliyopita huku mazungumzo yakiwa tayari yameanza.
No comments:
Post a Comment