KOCHA wa timu ya taifa ya Cameroon, Volker Finke anatarajiwa kuendelea kuinoa nchi hiyo kwa miaka mingine miwili baada ya mkataba wake kuongezwa leo. Shirikisho la Soka la nchi hiyo-Fecafoot lilikuwa halina mpango wa kumuongeza kocha huyo mwenye umri wa miaka 67 raia wa Ujerumani mkataba mpya na walikuwa tayri wameanza mchakato wakutafuta mbadala wake kabla ya kupewa amri ya kumuongeza mkataba mwingine. Vyombo vya habari vya Cameroon vimedai kuwa Finke anaungwa mkono na wadhamini wa jezi za nchi hiyo Puma ambao ndio wanaolipa mshahara wake wa dola 32,000 kwa mwezi pamoja na rais wan chi. Finke aliyekuwa mapumzikoni Ujerumani alirejea Cameroon wiki iliyopita ili kuwasilisha mipango yake ya maandalizi ya timu pamoja na kusaini mkataba huo mpya. Cameroon inatarajiwa kucheza mechi ya kimataifa ya kirafiki dhidi ya Burkina Faso Juni 6 jijini Paris kabla ya kupambana na Mauritania katika mchezo wa kufuzu michuano ya Mataifa ya Afrika 2017, Juni 12 mwaka huu.
No comments:
Post a Comment