Monday, June 22, 2015

DANI ALVES AMSIHI NEYMAR KUBADILI TABIA.

BEKI wa timu ya taifa ya Brazil, Dani Alves amebainisha kuwa amemhusia mchezaji mwenzake katika timu ya Barcelona Neymar kufuatia kutolewa katika mchezo waliochapwa bao 1-0 na Colombia katika michuano ya Copa America Jumatano iliyopita. Neymar mwenye umri wa miaka 23 alilimwa kadi nyekundu ya moja kwa moja wakati alipokwenda kumpiga kichwa golikipa wa Colombia Jeison Murillo baada ya mpira kumalizika kabla ya baadae kwenda kumzonga mwamuzi tena wakati wakielekea katika vyumba vya kubadilishia nguo. Kutokana na hilo Neymar amelimwa adhabu ya kutocheza mechi nne hivyo kumfanya kukosa mechi zote za michuano hiyo zilizobakia kama hata Brazil itafanikiwa kufika fainali. Akihojiwa Alves amesema alimwambia Neymar kuwa kimya na kujifunza kutokana na hilo ili asiweze kurudia tena kosa ambalo limeigharimu Brazil. Hata hivyo Alves anadhani adhabu kwa Neymar imekuwa kubwa sana kuliko angefanya mchezaji mwingine wa kawaida na pigo kubwa kumpoteza mchezaji muhimu kama huyo katika kikosi chao. Shirikisho la Soka la Brazil limethibitisha mapema leo kuwa Neymar anatarajiwa kuondoka katika kambi ya timu hiyo kufuatia uamuzi wa kutokata rufani kupinga adhabu hiyo.

No comments:

Post a Comment