Thursday, June 25, 2015

ETO'O NJIANI KWENDA UTURUKI.

MCHEZAJI bora wa zamani wa Afrika, Samuel Eto’o ameripotiwa kukubali kusajiliwa na klabu ya Antalyaspor ambaye imepanda katika Ligi Kuu ya Uturuki msimu huu. Klabu hiyo ilithibitisha kuwa wamefikia makubaliano na Eto’o lakini bado hawajasaini dili lolote rasmi. Katika taarifa yake, klabu hiyo imedai dili hilo limekwama kutokana na Eto’o kuwa na matatizo kuhusiana na haki za matangazo nchini Italia na pindi atakapomaliza ataelekea nchini humo kusaini mkataba. Mapema mwezi huu vyombo vya habari nchini Italia vilimkariri rais wa klabu ya Sampdoria Massimo Ferrro akidai kuwa anaamini mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 34 ataondoka ikiwa in miezi sita imepita toka atue Italia. Nahodha huyo wa zamani wa Cameroon amewahi kucheza katika klabu za Barcelona, Inter Milan, Chelsea na Everton huku akifanikiwa kunyakuwa tuzo mbili za mchezaji bora wa mwaka wa Afrika.

No comments:

Post a Comment