RAIS wa Barcelona, Josep Maria Bartomeu na bodi nzima ya klabu hiyo wanatarajiwa kuachia nyadhifa zao hizo leo ili kupisha uchaguzi mkuu kufanyika. Bartomeu aliitisha mkutano na wana habari leo ambapo atakabidhi madaraka kwa uongozi wa muda ambao ndio utakaopanga tarehe ya wagombea nafasi ya urais kuanza kampeni zao. Bartomeu mwenye umri wa miaka 52 amekuwa madarakani toka Sandro Rosell alipojiuzulu Januari mwaka 2014 kufuatia utata wa kifedha uliojitokeza wakati wa usajili wa Neymar. Utata huo pia ulimfanya Bartomeu na yeye kushitakiwa kea kosa la ukwepaji kodi na kulazimika kuitisha uchaguzi mapema Januari mwaka huu ili kukabiliana na mtikisiko huo uliojitokeza wakati huo. Bartomeu ambaye pamoja na mtikisiko huo klabu imefanikiwa kunyakuwa mataji matatu kwa msimu, anatarajiwa kugombea rasmi nafasi hiyo.
No comments:
Post a Comment