NYOTA wa kimataifa wa Argentina na klabu ya Barcelona Javier Mascherano amekanusha uvumi kuwa anataka kustaafu soka la kimataifa. Argentina walipoteza fainali yao ya pili kubwa ndani ya miezi 12 baada ya kutandikwa na Chile kwa changamoto ya mikwaju ya penati katika fainali ya Copa America, ikiwa umepita mwaka mmoja toka wafungwe tena na Ujerumani katika fainali ya Kombe la Dunia. Kufuatia kuvuma kwa tetesi hizo, Mascherano aliandika katika ukurasa wake wa mtandao wa kijamii wa twitter kuwa yote hayo yaliyosemwa juu yake sio ya kweli. Nyota huyo aliendelea kudai kuwa hana mpango wala hajawahi kufikiria kwasasa suala la kustaafu soka la kimataifa kwani bado anajiona kuna mchango anaweza kuendelea kutoa kwa nchi yake. Mascherano ameitumikia Argentina mechi 117 toka aitwe mara ya kwanza mwaka 2003 akiiwakilisha nchi yake katika michuano minne ya Copa America, mitatu ya Kombe la Dunia huku akifanikiwa kushinda medali ya thahabu katika michuano ya Olimpiki mwaka 2004 na 2008.
No comments:
Post a Comment