Thursday, July 9, 2015

KIVUMBI LIGI YA MABINGWA AFRIKA MWISHONI MWA WIKI HII.

MICHUANO ya Ligi ya Mabingwa ya Afrika inatarajiwa kuendelea mwishoni mwa wiki hii huku klabu za Entente Setif na TP Mazembe ambazo zinapewa nafasi kubwa ya kuibuka kidedea zikiwa na kibarua kizito cha kuhakikisha wanapata aama ugenini baada ya kuanza vibaya katika mechi zao za nyumbani. Mabingwa watetezi Setif wao walipoteza mchezo wao ka kutandikwa mabao 2-1 nyumbani na Waalgeria wenzake USM Alger wiki mbili zilizopita huku Mazembe wao waking’ang’aniwa sare ya bila kufungana na El Hilal ya Sudan. Kama hiyo haitoshi klabu hizo mbili zinakabiliwa na changamoto nyingine kwani wapinzani wao na wenyewe wanatafuta alama tatu kwa uchu mkubwa baada ya kupoteza michezo yao ya kwanza. Jumamosi Setif itapepetana na Mouloudia El Eulma klabu ya tatu kutoka Algeria iliyopo kundi B ambalo linakamilishwa na El Merreikh ya Sudan. Mazembe wao watasafiri mpaka Morocco kuifuata Moghreb Tetouan katika mchezo wa kundi A utakaofanyika Jumapili usiku. USM wao watakuwa na kibarua na Merreikh kesho katika mchezo utakaofanyika huko Algiers na Hilal watakuwa wenyeji wa Smouha ya Misri katika mchezo mwingine utakaochezwa Jumapili.

No comments:

Post a Comment