MSHAMBULIAJI nguli wa Uruguay Alcides Edgardo Ghiggia ambaye ndiye aliyeifungia timu yake bao la ushindi dakika 10 kabla ya mchezo kumalizika katika michuano ya Kombe la Dunia mwaka 1950, amefariki dunia. Ghiggia mchezaji pekee aliyekuwa amebaki hai kati ya wachezaji wote wa kikosi cha Uruguay ambacho kiliishinda Brazil katika mchezo fainali mwaka huo, ambapo dakika za lala salama zilimuingiza katika historia ya kuipatia ushindi nchi yake. Mchezaji huyo amefariki dunia akiwa na umri wa miaka 88 huku kifo chake kikitajwa kuwa ni pigo kubwa kwa Uruguay kwa kuondokewa na mtu mhimu katika historia ya soka lao. Ghiggia amefariki wakati taifa hilo likiadhimisha kumbukumbu ya miaka 65 tangu kufanyika kwa fainali hizo za Kombe la Dunia mwaka 1950 ambapo Uruguay iliibuka kidedea kupitia bao alilofunga. Ikumbukwe kwamba katika historia ya uwanja wa Maracana ni watu watatu tu waliofanikiwa kuunyamazisha uwanja huo, na enzi za uhai wake Ghiggia alinukuliwa akiwataja watu hao kuwa ni Papa, Muuimbaji Frank Sinatra na yeye mwenyewe.
No comments:
Post a Comment