RAIS wa klabu ya Valencia, Madeo Salvo(pichani kulia) amejiuzulu wadhifa wake huo jana akitoa sababu binafsi, ingawa vyombo vya habari nchini Hispania vimedai kuwa kuondoka kwake sambamba na maofisa wengine wanne kunatokana na kutoelewana na mmiliki wake Peter Lim (pichani kushoto). Salvo ambaye amekuwa rais wa Valencia toka mwaka 2013 sambamba na Lyhoon Chan ambaye ndio amechukua nafasi yake, amesema familia yake inapitia katika kipindi kigumu wakati huu. Akihojiwa Salvo amesema mwezi uliopita alimtahadharisha Chan kuwa pindi msimu wa La Liga utakapokwisha angependa kuachia nafasi yake hiyo ili aweze kushughulika na matatizo ya familia yake. Salvo aliendelea kudai kuwa baba yake anasumbuliwa na maradhi ya saratani hivyo haoni haja ya kuendelea kushikilia nafasi hiyo kama hawezi kujitoa kwa asilimia 100. Chan alimshukuru Salvo kwa utumishi wake na baadae kutangaza kuwa mbali na kuondoka kwake lakini pia maofisa wengine wanne nao wataondoka akiwemo mkurugenzi wa michezo.
No comments:
Post a Comment