KLABU ya Sporting Lisbon imetangaza kumsajili chipukizi mwenye kipaji kutoka Indonesia Martunis ambaye ni mhanga wa tetemeko la ardhi na tsunami iliyotokea mwaka 2004 katika mji wa Aceh. Akiwa na miaka nane Martunis alikuwa akicheza soka na marafiki zake wakati mafuriko hayo yalipotokea na kuwaua mama na dada zake huku yeye akisalimika kwa kushikilia vitu vilivyokuwa vikielea. Kwa siku 20 Martunis alikuwa akila vyakula ambavyo vilisombwa na maji kabla ya kuja kuokolewa na mwandishi wa habari wa Uingereza na kuonekana katika vyombo vya habri duniani kote. Picha za kijana huyo zilimvutia Cristiano Ronaldo ambapo yeye pamoja na baba yake walimsaidia kijana huyo kumaliza shule kabla ya kujiunga na akademi maarufu ya michezo nchini Ureno. Akihojiwa Martunis ambaye sasa ana miaka 17 aliishukuru akademi ya Sporting Lisbon kwa kumsaidia kutimiza ndoto zake na kuwataka vijana wenzake wengine kutokata tamaa.
No comments:
Post a Comment