Wednesday, July 1, 2015

UKAME WA MABAO WA MESSI HAUMUOGOPESHI KOCHA WA ARGENTINA.

KOCHA wa timu ya taifa ya Argentina, Gerardo Martino amesema Lionel Messi haitaji kufunga mabao ili awe na furaha baada ya mshambuliaji huyo wa kimataifa wa Barcelona kushindwa kufunga wakati walipoigaragaza Paraguay kwa mabao 6-1 jana. Katika mchezo huo wa nusu fainali ya michuano ya Copa America Messi alicheza katika nafasi ya kiungo na kusaidia kutengeneza mabao matano kati ya sita yaliyofungwa huku akitoa pasi za mwisho mara tatu. Akihojiwa Martino amesema kama Messi akitoa pasi ambazo mwisho wa siku zimezaa mabao hadhani kama kuna tatizo katika hilo kwani jinsi anavyomfahamu nyota huyo haitaji kufunga ili awe na furaha. Kocha huyo aliendelea kudai kuwa mara nyingi Messi hujali zaidi mafanikio ya timu kuliko yak wake binafsi. Argentina sasa watawavaa wenyeji wa michuano hiyo Chile katika mchezo wa fainali unaotarajiwa kuchezwa Jumamosi hii jijini Santiago.

No comments:

Post a Comment