Monday, August 3, 2015

BERLUSCONI AKUBALI KUIUZA AC MILAN.

WAZIRI mkuu wa zamani wa Italia, Silvio Berlusconi amesaini makubaliano ya mauzo ya awali ya hisa asilimia 48 za klabu ya AC Milan kwa kundi linaloongozwa na mfanyabiashara wa Thailand Bee Taechaubol. Msemaji wa kampuni ya Fininvest inayomilikiwa na Berlusoni amesema mpaka ifikapo Septemba 30 mwaka huu hisa hizo zitakuwa zimehamishwa sambamba na malipo ya euro milioni 480. Klabu ya AC Milan inamilikiwa na Fininvest, kampuni inayomilikiwa na familia ya Berlusconi ambayo pia inamiliki kituo cha luninga cha Mediaset na kampuni ya uchapishaji ya Mondadori. Msemaji huyo amesema dili hilo limesainiwa na Fininvest na Taechaubol na kuthibitishwa na Berlusconi mwenyewe. Naye mfanyabiashara huyo wa Thailand alithibitisha taarifa hizo kupitia ukurasa wake wa mtandao wa kijamii wa Instagram. Milan ambao ni mabingwa mara saba wa Ulaya, wamepoteza mng’aro wao katika miaka ya karibuni na kufanikiwa kushinda taji la mwisho la Serie A mwaka 2011. Klabu hiyo pia kwasasa inakabiliwa na madeni yanayofikia euro milioni 250 na mwaka jana wamepata hasara ya euro milioni 91.

No comments:

Post a Comment