Thursday, October 1, 2015

MATUNDA YA MKWASA YAANZA KUONEKANA BAADA YA TANZANIA KUANZA KUKWEA VIWANGO FIFA.

TANZANIA imekwea kwa nafasi nne katika viwango vipya vya Shirikisho la Soka Duniani-FIFA ambavyo hutolewa kila mwezi. Mwezi uliopita Tanzania ilikuwa katika nafasi ya 140 lakini katika viwango vipya vilivyotolewa leo imekwea mpaka nafasi ya 136 huku suala hilo likichagizwa zaidi na sare ya bila kufungana waliyopata Taifa Stars dhidi ya Nigeria. Stars ambayo inashika nafasi ya 42 kwa upande wa Afrika walipata sare hiyo katika mchezo wa kufuzu michuano ya Mataifa ya Afrika mwaka 2017 uliofanyika katika Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam mapema mwezi uliopita. Kwa upande wa Afrika Algeria wameendelea kuongoza kwa kushika nafasi ya 19 katika orodha ya viwango hivyo duniani wakifuatiwa na Ivory Coast wanaoshika nafasi ya 21 huku Ghana wao wakiwa nafasi ya tatu kwa kushika nafasi ya 25. Wengine ni Tunisia walioko nafasi ya 36 wakiwa wameporomoka kwa nafasi tatu na Senegal ndio wanaofunga orodha ya tano bora kwa upande wa Afrika kwa kushika nafasi ya 38. Kwa ujumla orodha hiyo mpya haina mabadiliko sana kwani Argentina bado wameendelea kuongoza wakifuatiwa na mabingwa wa dunia Ujerumani waliopanda kwa nafasi moja huku Ubelgiji wao wakiporomoka kwa nafasi moja mpaka ya tatu. Ureno wako katika nafasi ya nne baada ya kupanda kwa nafasi mbili na tano bora inafungwa na Colombia walioshuka nafasi moja.

No comments:

Post a Comment