Tuesday, October 6, 2015

NASRI AAPA KUTOICHEZEA UFARANSA TENA KATIKA MAISHA YAKE.

KIUNGO wa Manchester City, Samir Nasri amesisitiza kuwa hakuna kitu chochote kinachoweza kumfanya kuja kuichezea tena timu ya taifa ya Ufaransa. Nyota huyo wa zamani wa klabu za Marseille na Arsenal mara ya mwisho kuitumikia nchi yake ilikuwa mwaka 2013 lakini aliamua kuachana na soka la kimataifa baada ya kuachwa katika michuano ya Kombe la Dunia mwaka 2014 pamoja na kuwa sehemu muhimu katika kikosi cha City kilichonyakuwa taji la Ligi Kuu msimu wa 2013-2014. Nasri amekuwa na historia mbaya na Ufaransa kufuatia kuachwa pia katika michuano ya Kombe la Dunia mwaka 2010 kabla ya kusimamishwa na Shirikisho la Soka la nchi hiyo kwa kuzozana na wanahabari kufuatia kutolewa kwa Ufaransa katika hatua ya robo fainali ya michuano ya Euro 2012. Akihojiwa Nasri amesema hata kama baba yake ndio atakuwa kocha Ufaransa hatathubutu kurejea kuitumikia timu hiyo kutokana na mambo waliyomfanyia. Kiungo huyo amesema baada ya michuano ya Euro 2012 alitaka kuacha lakini baba yake alimwambia anatakiwa kucheza Kombe la Dunia na baada ya hapo alijaribu kuwa vizuri huku akijituma katika klabu yake lakini aliachwa. Nasri aliendelea kudai kuwa jambo lilimuudhi na akiwa kama binadamu akaamua kuchukua maamuzi na kutofiria masuala hayo na badala yake kuongeza nguvu katika klabu yake.

No comments:

Post a Comment