TIMU za Argentina na Brazil zimejiimarisha katika kampeni zao za kufuzu michuano ya Kombe la Dunia mwaka 2018 kwa kupata ushindi muhimu katika mechi zao za jana. Wakati wakongwe hao wakifanya vyema hali imekuwa ni tofauti kwa mabingwa wa michuano ya Copa America Chile kwa wamejikuta wakigaragazwa na Uruguay mabao 3-0. Argentina mabingwa mara mbili wa Kombe la Dunia, ambao waliambulia alama mbili katika mechi zao tatu za mwanzo jana walipata ushindi wao wa kwanza kwa kuichapa Colombia bao 1-0 katika mchezo uliofanyika huko Baranquilla. Kwa upande wa Brazil wao waliigaragaza Peru kwa mabao 3-0 ambayo yaliwekwa kimiani na nyota wa Bayern Munich Douglas Costa aliyefunga moja na kutengeneza mengine mawili. Ushindi huo wa Uruguay unawafanya kukwea mpaka nafasi ya pili katika msimamo wakiwa na alama tisa katika mechi nne, wakifuatiwa na Brazil waliopo nafasi ya tatu wakiwa na alama saba huku Argentina wao wakikwea mpaka nafasi sita.
No comments:
Post a Comment