MCHEZO wa kirafiki wa kimataifa kati ya Ubelgiji na Hispania uliotarajiwa kuchezwa baadae leo jijini Brussels umefutwa kwasababu ya wasiwasi wa masuala ya kiusalama kufuatia mashambulio ya mauaji yaliyofanyika jijini Paris. Jumla ya watu 129 waliuawa katika shambulio hilo lililofanyika Ijumaa iliyopita, ambalo pia lililenga mchezo wa kirafiki kati ya Ufaransa na Ujerumani uliokuwa ukifanyika Stade de France. Waendesha mashitaka nchini Ufaransa wameng’amua kuwa raia mmoja wa Ubelgiji ndio aliyepanga mashambulio hayo. Shirikisho la Soka la Ubelgiji limedai kuwa limechukua uamuzi huo wa kusitisha mchezo huo uliokuwa umepangwa kuchezwa katika Uwanja wa King Baudouin, kufuatia kushauriana na viongozi wa Hispania. Taarifa ya shirikisho hilo iliendelea kwa kuomba radhi mashabiki wa soka na kuongeza kuwa hawakupenda kuweka maisha ya wachezaji na mashabiki wao hatarini ndio maana wakafikia uamuzi huo.
No comments:
Post a Comment