MENEJA wa zamani wa Real Madrid, Rafael Benitez amefunguka kwa kuishukuru klabu hiyo kwa kumpa nafasi na kumtakia kila la kheri mrithi wake Zinedine Zidane. Benitez alitimuliwa Jumatatu baada ya kupita miezi saba toka akabidhiwe mikoba ya kuinoa timu hiyo na nafasi yake kuchukua nguli wa klabu hiyo Zidane ambaye alikuwa akikinoa kikosi B cha Castilla. Kuanza kampeni za msimu huu kwa kusuasua kikiwemo na kipigo cha mabao 4-0 kutoka mahasimu wao Barcelona kulichangia kwa kiasi kikubwa kutimuliwa kwa Benitez, huku mgomo baridi katika vyumba vya kubadilishia nguo nao ukitajwa kuchangia pia. Lakini katika taarifa yake aliyotoa katika matandao wake, Benitez amewahakikishia kuwa hana kinyongo chochote kufuatia kutimuliwa kwake. Benitez amesema imekuwa ni heshima kubwa kwake kupata nafasi ya kuinoa klabu hiyo hivyo anawashukuru viongozi, wafanyakazi, wachezaji na mashabiki kwa kumuunga kwao mkono katika kipindi chote alichokuwepo Santiago Bernabeu.
No comments:
Post a Comment