KOCHA wa timu ya taifa ya Italia, Antonio Conte ambaye anatarajiwa kuchukua mikoba ya kuinoa Chelsea kipindi hiki cha kiangazi, amefutiwa mashitaka ya upangaji matokeo yaliyokuwa yakimkabili. Conte alikuwa mmoja wa washitakiwa kadhaa katika kesi hiyo iliyokuwa ikisikilizwa huko Cremona ikihusisha wakati akiifundisha klabu ya Siena ambayo wakati huo ilikuwa ikicheza Serie B. Meneja huyo mwenye umri wa miaka 46 alikuwa akituhumiwa kwa kushindwa kutoa taarifa ya jinsi anavyofahamu suala la kupanga matokeo kwa wachezaji katika kipigo cha bao 1-0 walichopata kutoka kwa Albinoleffe Mei mwaka 2011. Mwendesha mashitaka Roberto Di Martino alikuwa amependekeza adhabu ya kifungo cha miezi sita jela na faini ya euro 8,000 kwa meneja huyo wa zamani wa Juventus lakini aliachiwa huru mapema leo. Conte anatarajiwa kuchukua nafasi ya meneja wa muda wa Chelsea Guus Hiddink baada ya kumalizika michuano ya Euro 2016.
No comments:
Post a Comment