Thursday, June 9, 2016

RONALDO NA MESSI NDIO WANAMICHEZO WANAOLIPWA ZAIDI ULIMWENGUNI.

JARIDA maarufu la Forbes la Marekani limewataja wachezaji nyota Cristiano Ronaldo na Lionel Messi kuwa ndio wanamichezo wanaolipwa zaidi duniani. Nyota wa Real Madrid Ronaldo ndio anaongoza orodha hiyo kwa kukunja kitita cha paundi milioni 60.9 katika kipindi cha miezi 12 iliyopita huku nyota wa Barcelona Messi yeye akijikusanyia paundi milioni 56.3. Nyota wa mchezo wa gofu Tiger Woods na bondia Floyd Mayweather ndio waliokuwa wakitawala orodha hizo kwa muongo mmoja uliopita lakini huku Woods akiandamwa na majeruhi na kushuka kiwango na Mayweather akiwa amestaafu Ronaldo na Messi wamepanda na kuongoza orodha hizo. Ronaldo anakuwa mwanamichezo wa pili kutoka katika timu baada ya nguli wa mpira wa kikapu Michael Jordan kuongoza orodha hizo toka jarida hilo lilipoanza kukokotoa vipato vya nyota vya wanamichezo mbalimbali mwaka 1990. Nyota wengine waliopo katika orodha hiyo ni nyota wa mpira wa kikapu Lebrone James anayeshika nafasi ya tatu kwa kuingiza paundi milioni 53.4, nyota wa tenisi Roger Federer yuko nafasi ya nne akiingiza paundi milioni 46.9 na nyota mwingine wa mpira wa kikapu Kevin Durant anakamilisha tano bora kwa kuingiza paundi milioni 38.6. Neymar, Zlatan Ibrahimovic na Gareth Bale ndio wachezaji soka wengine pekee waliopo katika orodha hiyo wakiwa katika nafasi ya 21, 22 na 25 kwa kuingiza kiasi cha paundi milioni 25.8, 25.7 na 24.7.

No comments:

Post a Comment