Friday, June 10, 2016

PLATINI ANATEGEMEA REKODI YAKE YA MABAO EURO ITAVUNJWA MWAKA HUU.

RAIS wa zamani wa Shirikisho la Soka la Ulaya-UEFA, Michezo Platini anategemea rekodi yake ya kufunga mabao tisa katika mashindano ya Ulaya itavunjwa mwezi huu katika michuano hiyo inayotarajiwa kuanza kutimua vumbi Ufaransa. Platini mwenye umri wa miaka 60, amewahi kucheza mara moja pekee lakini alimaliza akiwa mfungaji kinara akiwa na mabao tisa katika mechi tano alizocheza katika michuano ya mwaka 1984 ambapo Ufaransa waliibuka mabingwa katika ardhi yao ya nyumbani. Kueleka katika michuano ya mwaka huu, nyota wa Ureno Cristiano Ronaldo na Zlatan Ibrahimovic wa Sweden ndio wanaopewa nafasi kubwa ya kuipita rekodi hiyo, baada ya wachezaji hao kufunga mabao sita kila mmoja katika fainali tatu zilizopita. Platini aliifungia Ufaransa mabao 41 na kutwaa tuzo tatu za Ballon d’Or lakini rekodi hizo tayari zimeshafutwa na mshambuliaji wa zamani wa Arsenal, Thierry Henry na nyota wa Barcelona Lionel Messi. Akihojiwa, Platini ambaye liwahi kuichezea Juventus enzi zake, anaamini rekodi yake hiyo ya mabao nayo inaweza kuvunjwa katika michuano ya safari hii.

No comments:

Post a Comment