KIUNGO wa Manchester City, Yaya Toure amejitokeza na kuomba radhi kwa wasimamizi wa klabu hiyo baada ya kutochezeshwa kwa muda na meneja Pep Guardiola. Nyota huyo aliomba radhi kupitia ukurasa wake wa mtandao wa kijamii wa Facebook, akidai kuwa kauli ya wakala wake haiwakilishi msimamo wake kuhusu klabu au watu wanaofanya kazi hapo. Wiki iliyopita, Guardiola aliwaambia wanahabari kuwa anahitaji kumtumia Toure katika kikosi chake lakini bado anasubiria kuombwa radhi na wakala wa cmhezaji huyo Dimitri Seluk. Seluk alimjia juu Guardiola baada ya meneja huyo kumuacha Toure katika kikosi cha Ligi ya Mabingwa Ulaya, akidai kuwa meneja huyo atapaswa kumuomba radhi mteja wake kama City ikishindwa kutwaa taji hilo. Kufuatia kauli hiyo, Guardiola alijibu kwa kueleza kuwa kamwe hatamtumia Toure katika kikosi chake mpaka wakala huyo atakapomuomba radhi.
No comments:
Post a Comment