MABINGWA wa soka wa Afrika, Mamelodi Sundowns ya Afrika Kusini wametolewa katika hatua ya robo fainali ya michuano ya Klabu Bingwa ya Dunia inayoendelea huko nchini Japan. Sundowns walitandikwa mabao 2-0 na timu ya Kashima Antlers katika mchezo uliofanyika jijini Osaka mapema leo. Klabu hiyo ilikuwa inashiriki michuano hiyo kwa mara ya kwanza baada ya kutwaa taji la Ligi ya Mabingwa Afrika kwa mara ya kwanza katika historia yao. Sundowns sasa inatarajiwa kucheza na Jeonbuk Hyundai ya Korea Kusini katika mchezo wa kutafuta mshindi wa tano Jumatano ijayo huku Kashima wao wakicheza na Atletico Nacional ya Colombia katika hatua ya nusu fainali. Mabingwa wa Ulaya Real Madrid wao wanatarajiwa kutua nchini Japan mapema kesho kwa ajili ya mchezo mwingine wa nusu fainali dhidi ya Club America ya Mexico utakaochezwa Alhamisi. Michuano hiyo hushirikisha mabingwa kutoka mabara sita pamoja na nchi mwenyeji.

No comments:
Post a Comment