Friday, August 4, 2017

COSAFA WAIPA TAIFA STARS ZAWADI ZAO

BARAZA la Mpira wa Miguu kwa Nchi za Kusini mwa Afrika (Cosafa), limetoa zawadi ya dola 10,000 kwa Taifa Stars ya Tanzania baada ya kushinda na kushika nafasi ya tatu katika mashindano ya Castle Cosafa yaliyofanyika mwezi uliopita nchini Afrika Kusini. Fedha hizo ni sawa na Sh. 22,000,000 ambako Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), limeamua fedha hizo kwa mgawanyo sawa, zitolewe kwa wachezaji wote walioshiriki fainali hizo pamoja na benchi la ufundi. Kadhalika Cosafa limetuma fedha za zawadi kwa wachezaji wa Tanzania ambao walifanya vema kwenye mchezo mmoja baada ya mwingine katika mashindano hayo ambayo yalikuwa na mvutio wa aina yake kwa mafanikio ya timu ya Tanzania. Wachezaji hao ni Shiza Kichuya aliyeibuka Mchezaji Bora wa mechi kati ya Tanzania na Malawi; Muzamiru Yassin aliyeibuka Mchezaji Bora wa mechi kati ya Tanzania na Angola; Erasto Nyoni aliyeibuka Mchezaji Bora wa mechi kati ya Tanzania na Mauritius; Elius Maguri aliyeibuka Mchezaji Bora wa mechi kati ya Tanzania na Afrika Kusini. Kipa Bora wa michuano hiyo ni Said Mohammed alyezawadiwa moja kwa moja na Cosafa. Tanzania ilishika nafasi ya tatu nyuma ya mabingwa Zimbabwe na Zambia iliyoshika nafasi ya pili. Tanzania iliifunga Lesotho na kushika nafasi ya tatu.

No comments:

Post a Comment