
Tuesday, April 3, 2012
SAFA YAZIDAI MIJI WENYEJI WA AFCON RANDI MILIONI 22.
CHAMA cha Soka nchini Afrika Kusini-SAFA kinadai kiasi cha randi milioni 22 kwa kila mji utakaotumika kama mwenyeji wa mashindano ya Kombe la Mataifa ya Afrika itakayofanyika mwakani. SAFA kinatafuta fedha kwa ajili ya kufidia gharama ya michuano hiyo ambayo inatarajiwa kutumia kiasi cha zaidi ya randi milioni 100 ambapo miji hiyo saba itakayokuwa mwenyeji itatakiwa kulipa kiasi hicho au watanyimwa nafasi hiyo. Suala hili lilijulikana baada ya jiji la Cape Town kutaka kujitoa katika kinyang’anyiro cha kuwa mwenyeji kwasababu hawataki kutumia pesa za walipa kodi wao kwa ajili mpira. Diwani wa jiji la Cape Town Grant Pascoe amesema mji wake huo una nia ya kuwa mwenyeji wa michuano hiyo ndio maana wametuma barua ya maombi lakini kwa kiwango ambacho SAFA wanadai hawataweza kukimudu.
BEKI WA ATALANTA AKAMATWA KWA KASHFA YA UPANGAJI MATOKEO.
BEKI wa Atalanta, Andrea Masiello amekamatawa baada ya taarifa kwamba alihusika na upangaji wa matokeo na wachezaji wenzake wanane wa zamani wa Bari na suala lao lipo chini ya uchunguzi. Taarifa iliyotolewa na Shirikisho la Soka Italia imesema kuwa upangaji wa matokeo unazorotesha maendeleo ya soka nchini humo na wameahidi kuchukua hatua kwa atakayekutwa na hatia. Tangu kundi la kwanza la watu 16 wakamatwe Juni, mwaka jana, watu wengine 30 wamekamatwa, akiwemo nahodha wa zamani wa Atalanta, Cristiano Doni na nahodha wa zamani wa Lazio, Giuseppe Signori. Mechi tisa za mwisho za Bari msimu uliopita zinachunguzwa, kwa mujibu wa shirikisho, ikiwemo mechi ambayo bao la kujifunga la Masiello liliisaidia Lecce kushinda 2-0 na kuepuka kushuka daraja, baada ya Bari kuwa tayari imeshuka.
UONGOZI WA AL WASL WAMKINGIA KIFUA MARADONA.
KLABU ya Al Wasl ya Dubai imesema kwamba kocha wao, Diego Maradona alifanya jambo la heshima baada ya kuteremika jukwaani kuwavaa mashabiki waliokuwa wanamzomea mpenzi wake na wake za wachezaji wa klabu hiyo. Al Wasl imesema kwenye tovuti ya klabu hiyo leo kwamba hasira za Maradona zilikuwa zinaeleweka na alifanya jambo la heshima mwishoni mwa wiki. Abdullah al-Bishr pia alimuomba radhi gwiji huyo wa Argentina, ambaye alianza kuifundisha timu hiyo mwaka jana. Maradona alipambana na mashabiki wa timu pinzani, Al Shabab ambao waliwazomea wanawake wa wachezaji wa timu yake ambayo katika mchezo huo walifungwa mabao 2-0. Maradona aliwaita mashabiki wa Al Shabab ni waoga.
Monday, April 2, 2012
WENGER AKUNWA NA TAARABT.
KOCHA wa Arsenal, Arsene Wenger anaamini kiungo wa timu ya Queens Park Rangers, Adel Taarabt ana kila kitu cha kuitwa mchezaji bora lakini kwa sasa anahitaji kufanya vizuri zaidi kila wiki wakati timu yake ikicheza. Taarabt ndio alifunga bao lililoipa ushindi timu yake dhidi ya Arsenal Jumamosi kwenye Uwanja wa Loftus Road bao ambalo ni kwanza kwa mchezaji huyo katika msimu huu wa Ligi Kuu nchini humo. Mwanasoka huyo wa kimataifa wa Morocco, alikuwa chachu ya timu yake kupanda Ligi Kuu msimu uliopita, akiifungia mabao 19 na Wenger amesema kijana huyo mwenye umri wa miaka 22 sasa anatakiwa kudumisha ubora wake uwanjani. Wenger alimsifu kinda huyo kwamba ana kipaji cha hali ya juu na ameonyesha hilo kwenye mchezo huo lakini akasisitiza kuwa bado ana safari ndefu ya kuelekea mafanikio kwasababu anahitaji kucheza kwa kiwango cha juu mfululizo.
SIMBA WAONDOKA LEO KUIFUATA EL-SETIF.
WAWAKILISHI pekee wa Tanzania katika michuano ya Afrika, Simba SC wameondoka alfajiri ya leo Dar es Salaam kuelekea Algeria kwa ajili ya mechi ya marudiano, Raundi ya Pili Kombe la Shirikisho la Soka Afrika dhidi ya wenyeji ES Setif, wakipitia Algeria. Simba imeondoka nchini huku wakiwa na matumaini makubwa ya kuitoa ES Setif katika mchezo huo utakaofanyika Ijumaa wiki hii. Ofisa Habari wa Simba, Ezekiel Kamwaga alisema wachezaji wapo katika hali nzuri na kwamba wimbo wao ni ushindi, huku akiwataja viongozi watakaofuatana na timu hiyo kuwa ni Mwenyekiti wa klabu hiyo, Ismail Aden Rage, Mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya klabu hiyo Damian Manembe na Kamwaga. Amesema benchi la ufundi watakaokuwepo ni Kocha Mkuu Milovan Cirkovic, Kocha Msaidizi Amatre Richard, kocha wa makipa James Kisaka, daktari wa timu Cosmas Kapinga, Nyagawa na mtunza vifaa Kessy Rajab. Aliwataja wachezaji waliopo kwenye msafara kuwa ni Juma Kaseja, Ally Mustafa, Nassor Masoud, Shomari Kapombe, Amir Maftaha, Juma Nyoso, Kelvin Yondani, Victor Costa, Obadia Mungusa, Jonas Mkude, Patrick Mafisango, Mwinyi Kazimoto, Haruna Moshi, Salum Machaku, Uhuru Suleiman, Felix Sunzu, Emmanuel Okwi, Edward Christopher, Derick Walulya na Gervais Kago.
NYOTA WA ZAMANI WA LAZIO AFARIKI DUNIA.
MCHEZAJI nyota wa zamani kimataifa wa Italia ambaye amewahi pia kuzichezea klabu za Lazio na New York Cosmos, Giorgio Chinaglia amefariki dunia kutokana na matatizo ya ugonjwa wa moyo. Katika taarifa iliyotolewa na mtoto wa kiume wa mchezaji huyo aitwae Antony amesema kuwa Chinaglia alifariki akiwa nyumbani kwake Naples, Florida, Marekani ambapo alikuwa akifanya kazi katika kituo kimoja cha radio nchini humo. Klabu ya Lazio pia ilitangaza kifo cha Chinaglia ambaye alikuwa akiishi Marekani toka alipotuhumiwa kushirikiana na kikundi cha wahalifu ambao walikuwa wakitaka kuinunua Lazio mwaka 2006. Chinaglia aliisaidia Lazio kushinda taji lake la kwanza la Ligi Kuu nchini Italia mwaka 1974 ambapo baadae aliteuliwa kuwa rais wa klabu hiyo. Mwaka 1976 alijiunga na klabu ya Cosmos ya Marekani akicheza pamoja na gwiji wa soka wa Brazil Pele pamoja na nyota wa Ujerumani enzi hizo Franz Beckenbauer na pia aliwamo katika kikosi cha Italia kilichoshiriki michuano ya Kombe la Dunia mwaka 1974.
IRAQ KUIANGUKIA FIFA.
SHIRIKISHO la Soka la Iraq-IFA limelitaka Shirikisho la Soka Duniani-FIFA kuwafungulia ili waweze kucheza michezo ya kirafiki ya kimataifa katika uwanja wao wa nyumbani. Makamu wa rais wa IFA Abdel Khaleq Massoud amesema kuwa watajaribu kuishawishi FIFA kwa kuwapelekea ushahidi kwamba nchi hiyo iko salama kuandaa michezo ya kirafiki. Massoud amesema kuwa rais wa IFA Najeh Hmoud anatajiwa kuongoza jopo la viongozi watakaokwenda kuonana na rais wa FIFA Sepp Blatter jijini Zurich April 13 mwaka huu kuongelea mustakabali wa soka la nchi hiyo. Aliongeza kuwa jopo hilo litajaribu kuiomba FIFA kuwafungulia ili waweze japo kuandaa michezo ya kimataifa ya kirafiki ya timu ya taifa ya nchi hiyo katika uwanja wa nyumbani wakati wakiendelea kuwafungia kucheza michezo ya mashindano nyumbani. FIFA iliifungia Iraq kuandaa michezo katika viwanja vyake vya nyumbani kufuatia vurugu zilizotokea Septemba 2 mwaka jana katika mji wa Kurdistan.
Subscribe to:
Posts (Atom)