Thursday, August 2, 2012

SUAREZ AWAPONDA MASHABIKI WANAOMZOMEA.

MSHAMBULIAJI wa kimataifa wa Uruguay, Luis Suarez amewaponda mashabiki ambao walikuwa wakimzomea wakati timu yake ilipokubali kipigo cha bao 1-0 dhidi ya Uingereza katika michuano ya Olimpiki akidai kuwa ni dalili za mashabiki hao kumhofia. Suarez ambaye anacheza katika klabu ya Liverpool alichukizwa na kitendo kilichoonyeshwa na mashabiki waliojitokeza katika Uwanja wa Millennium ambao walikuwa wakidhihaki wimbo wa taifa wa Uruguay ulipokuwa ukipigwa kabla ya kuanza kwa mchezo baina ya timu hizo. Suarez amesema kuwa mashabiki kumdhihaki na kumzomea yeye hilo halikuwa tatizo kwake lakini kitendo kilichoonyeshwa na mashabiki hao wakati wimbo wa taifa wa nchi yake hakikuwa kitendo cha uungwana na hakikupaswa kutokea. Mchezaji huyo amekuwa akizomewa mara kwa mara nchini Uingereza kutokana na tukio lake la kumtupia maneno ya kibaguzi beki wa klabu ya Manchester United Patrice Evra wakati timu hizo zilipokutana katika mchezo wa Ligi Kuu nchini Uingereza ambapo alipewa adhabu ya kufungiwa michezo nane na faini kwa tukio hilo.

YANG AAMUA KUACHANA NA VINYOYA.

Yu Yang.
MCHEZAJI wa mchezo wa vinyoya au badminton, Yu Yang ambaye ni mmoja kati ya wachezaji ambaye aliondolewa katika michuano ya Olimpiki amesema kuwa ameamua kuchana na mchezo huo. Yang na mchezaji mwenzake Xiaoli Wang walienguliwa na Shirikisho la Dunia la mchezo huon jana kutokana na kile kilichodaiwa kupanga matokeo kutokana na kuonekana wakicheza chini ya kiwango. Maofisa wa olimpiki kutoka China walidai kuwa wachezaji hao walitafakari kwa undani juu ya suala hilo na wanaomba msahamaha. Yang alituma ujumbe katika mtandao wa kijamii wa twitter akisema kuwa hiyo ni mara yake ya mwisho kushiriki mashindano hayo na kuwaaga mashabiki wake. Wachezaji wawili wa Korea Kusini na mmoja kutoka Indonesia nao pia waliondolewa katika michezo ya juzi kutokana na makosa kama kama hayo.

MISRI, SENEGAL ZATINGA ROBO FAINALI OLIMPIKI.

WAWAKILISHI wa Afrika katika soka kwenye michuano ya Olimpiki inayoendelea jijini London timu za Misri na Senegal zimefanikiwa kusonga mbele katika michuano hiyo baada ya kutinga hatua ya robo fainali. Misri waliingia katika hatua baada ya kuichapa bila ya huruma timu ya Belarus kwa mabao 3-1 na kutinga hatua hiyo ambapo sasa watakutana na timu ya Japan katika mchezo utakaochezwa Juamosi katika Uwanja wa Old Traford jijini Manchester. Senegal nao walitinga hatua hiyo baada ya kutoa sare ya bao 1-1 dhidi ya Umoja wa Falme za Kiarabu-UAE bao ambalo lilisawazishwa na mshambuliaji nyota wa timu hiyo Moussa Konate ambapo mpaka sasa amefunga mabao manne katika michuano hiyo. Nchi hiyo sasa itapambana na Mexico ambao wanaongoza kundi B baada ya kuibuka na ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Switzerland huku wenyeji wa michuano hiyo Uingereza wenyewe watacheza na Korea Kusini. Timu inayopewa nafasi kubwa ya kunyakuwa medali ya dhahabu kwa mara kwanza katika michuano hiyo Brazil wenyewe watamenyana na Honduras katika robo fainali ya michuano hiyo.

Wednesday, August 1, 2012

CARROLL AJUMUISHWA KIKOSI CHA LIVERPOOL.

Andy Carroll.
MSHAMBULIAJI wa klabu ya Liverpool Andy Carroll ameitwa katika kikosi cha timu hiyo ambacho kitacheza mchezo wa kufuzu kwa ajili ya michuano ya Kombe la Ligi ya Ulaya maarufu kama Europa League dhidi ya timu ya FC Gomel kesho ingawa hatma yake bado haijajulikana. Mshambuliaji huyo wa kimataifa wa Uingereza kushiriki kwake kwenye mchezo huo utakaochezwa chini Belarus hautaathiri uwezekano wake wa kutumiwa katika mashindano mengine. Hatahivyo klabu ya West Ham bado wana matumaini ya kupata saini ya Carroll ingwa wamekiri kimya kimya kwamba wanaweza kushindw mbio hizo baada ya Newcastle nao kuingia katika kinyang’anyiro hicho. Sheria za Shirikisho la Soka Duniani-UEFA linaruhusu mchezaji kucheza mchezo wa kufuzu michuano ya Europa League na baadae kuhamia klabu nyingine kucheza michezo ya hatua makundi.

VILLA KUREJEA UWANJANI KARIBUNI.

David Villa.
DAKTARI wa klabu ya Barcelona, Ramon Cugat amesema kuwa mshambuliaji nyota wa timu hiyo David Villa amepona mguu wake ambao ulivunjika. Mshambuliaji huyo wa kimataifa kutoka Hispania amkuwa nje ya uwanja toka alipofanyiwa upasuaji Desemba mwaka jana lakini mchezaji huyo bado anahitaji muda zaidi ili aweze kupona kwa asilimia mia moja. Barcelona walipata tabu bila ya kuwepo kwa Villa mwenye umri wa miaka 30 msimu uliopita ingawa timu ya taifa ya Hispania yenyewe ilifanikiwa kutetea taji lake la Ulaya bila ya kuwepo mshambuliaji huyo anayeoongoza kwa mabao katika kikosi hicho. Daktari huyo pia amesema kuwa kiungo Thiago Alcantara na Isaac Cuenca bado hawajapona majeraha yanayowasumbua. Barcelona inatarajiwa kucheza mchezo wake wa kwanza Agosti 19 dhidi ya Real Sociedad katika Ligi Kuu nchini Hispania inayojulikana zaidi kama La Liga.

SHEWEN ANYAKUWA DHAHABU NYINGINE.

Yen Shuwen.
MUOGELEAJI kinda kutoka China Yen Shiwen ameshinda medali yake ya pili ya dhahabu ya mita 200 katika michuano ya kuogelea ya Olimpiki inayoendelea jijini London. Shiwen mwenye umri wa miaka 16 ambaye alishinda medali ya dhahabu pia katika mashindano hayo ya mita 400 kwa kutumia muda wa dakika 7.57 na kuweka rekodi ya muda wa kasi zaidi katika michuano hiyo. Katika mashindano hayo Alicia Coutts alishika nafasi ya pili na kupewa medali ya fedha akitumia muda wa dakika 2.08.15 wakati Caitlin Leverenz wa Marekani alishinka nafasi ya tatu na kupata medali ya shaba akitumia muda wa dakika 2.08.95. Katika michuano hiyo China inaongoza kwa kunyakuwa medali nyingi zaidi ikiwa imejikusanyia medali 23, dhahabu 13 fedha sita na shaba nne, nchi inayofuatia ni Marekani nayo ikiwa na idadi sawa ya medali 23 lakini wenyewe wakiwa na dhahabu tisa fedha nane na shaba sita. Nchi ya tatu kwa wingi wa medali mpaka sasa ni Ufaransa ambayo imenyakuwa medali 11, medali nne za dhahabu, tatu za fedha na nne za shaba.

TAARIFA KUTOKA TFF: CHUJI, BAHANUZI WAITWA TAIFA STARS.

WACHEZAJI 21 WATEULIWA KIKOSI CHA TAIFA STARS
Kocha Mkuu wa Taifa Stars, Kim Poulsen leo (Agosti 1 mwaka huu) ametangaza kikosi cha wachezaji 21 kwa ajili ya mechi ya kirafiki itakayochezwa ugenini Agosti 15 mwaka huu. Wachezaji walioitwa Taifa Stars inayodhaminiwa na Kilimanjaro Premium Lager wanatakiwa kuripoti kambi kwenye hoteli ya Tansoma, Dar es Salaam, Agosti 8 mwaka huu saa 1 jioni tayari kwa mazoezi yatakayoanza siku inayofuata. Makipa walioitwa kwenye kikosi hicho ni Deogratias Munishi (Azam), nahodha Juma Kaseja (Simba) na Mwadini Ali (Azam). Mabeki ni nahodha msaidizi Aggrey Morris (Azam), Erasto Nyoni (Azam), Kelvin Yondani (Yanga) na Shomari Kapombe (Simba). Viungo ni Athuman Idd (Yanga), Frank Domayo (Yanga), Haruna Moshi (Simba), Mrisho Ngassa (Azam), Mwinyi Kazimoto (Simba), Ramadhan Chombo (Azam), Ramadhan Singano (Simba), Salum Abubakar (Azam) na Shabani Nditi (Mtibwa Sugar). Wachezaji wanaounda safu ya ushambuliaji ni John Bocco (Azam), Mbwana Samata (TP Mazembe, Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo- DRC), Said Bahanuzi (Yanga), Simon Msuva (Yanga) na Thomas Ulimwengu (TP Mazembe, Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo- DRC).