Sunday, February 3, 2013

TAARIFA MBALIMBALI KUTOKA TFF LEO.

PAMBANO LA YANGA, MTIBWA SUGAR LAINGIZA MIL 125/-
Mechi namba 100 ya Ligi Kuu ya Vodacom iliyochezwa jana (Februari 2 mwaka huu) Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam na kumalizika kwa timu hizo kutoka sare ya bao 1-1 limeingiza sh. 125,181,000. Watazamaji 22,030 walikata tiketi kushuhudia mechi hiyo iliyochezwa kwa viingilio vya sh. 5,000, sh. 8,000, sh. 15,000 na sh. 20,000 huku kila klabu ikipata mgawo wa sh. 30,356,002.45 wakati Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) iliyolipwa ni sh. 19,095,406.78. Kiingilio cha sh. 5,000 ndicho kilichovutia watazamaji wengi ambapo 19,583 walikata tiketi hizo na kuingiza sh. 97,915,000. Mgawo mwingine wa mapato hayo ni asilimia 15 ya uwanja sh. 15,435,255.48, tiketi sh. 3,183,890, gharama za mechi sh. 9,261,153.29, Kamati ya Ligi sh. 9,261,153.29, Mfuko wa Maendeleo ya Mpira wa Miguu (FDF) sh. 4,630,576.64 na Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Dar es Salaam (DRFA) sh. 3,601,559.61.

WANYARWANDA KUCHEZESHA MECHI YA STARS, CAMEROON
Waamuzi kutoka Rwanda wanaotambuliwa na Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Miguu (FIFA) ndiyo watakaochezesha pambano katika Tanzania na Cameroon litakalochezwa Jumatano kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam. Mwamuzi wa katikati atakuwa Munyemana Hudu wakati wasaidizi wake ni Simba Honore na Ndagizimana Theogine wakati mwamuzi wa mezani ambaye pia anatambuliwa na FIFA atakuwa Oden Mbaga wa Tanzania. Hudu na wenzake watawasili nchini kesho (Februari 4 mwaka huu) saa 12.40 jioni kwa ndege ya RwandAir na wamepangiwa kufikia kwenye hoteli ya JB Belmont. Mechi ambayo ni moja kati ya nyingi zitakazochezwa siku hiyo (FIFA Date) itafanyika kuanzia saa 11 kamili jioni.

KUNDI LA AKINA ETO’O KUTUA KESHO DAR
Wakati kundi la kwanza la timu ya Cameroon lenye watu 13 linaingia nchini leo (Februari 3 mwaka huu) saa 4.40 usiku, kundi la pili linaloongozwa na nahodha wa timu hiyo Samuel Eto’o linatua kesho (Februari 4 mwaka huu) saa 3.45 asubuhi kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA). Eto’o anayechezea timu ya Anzhi Makhachkala ya Urusi atatua kwa ndege ya Kenya Airways akiwa na Herve Tchami wa Budapest Honved ya Hungary, beki Nicolas Nkoulou wa Marseille ya Ufaransa, mshambualiji Jean Paul Yontcha wa SC Olhanense ya Ureno na daktari wa timu Dk. Boubakary Sidik. Saa moja baadaye baada ya Eto’oo kutua na wenzake, Kocha wa timu hiyo Jean Paul Akono na msaidizi wake Martin Ndtoungou watawasili saa 4.40 asubuhi kwa ndege ya Kenya Airways wakitokea Afrika Kusini. Kesho pia kuna kundi lingine litakaloingia saa 4.40 usiku kwa ndege ya KLM ambalo lina beki Jean Kana Biyick wa Rennes ya Ufaransa, mshambuliaji Fabrice Olinga wa Malaga FC ya Hispania, beki Allan Nyom wa Udinese ya Italia ambaye yuko kwa mkopo Granada ya Hispania na beki wa kushoto Henri Bedimo wa Montpellier ya Ufaransa. Wachezaji waliobaki wakiongozwa na kiungo wa Barcelona, Alexandre Song watawasili Februari 5 mwaka huu kwa muda tofauti kwa ndege za KLM na Kenya Airways.

GAZZA AHITAJI MSAADA WA HARAKA KUTOKANA NA MATATIZO YA ULEVI YANAYOMSUMBUA.

WAKALA wa kiungo wa zamani wa kimataifa wa Uingereza Paul Gascoigne maarufu kama Gazza anaamini kuwa maisha ya nyota huyo yako hatarini baada ya kuanza tena ulevi wa kupitiliza. Gazza ambaye amewahi kusumbuliwa na matatizo ya unywaji wa pombe uliopitiliza na kulazwa katika hospitali moja ya waginjwa wa akili miaka mitano iliyopita, alionekana kuwa katika hali ya kilevi wakati wa shughuli za kijamii jijini Northampton Alhamisi iliyopita. Wakala wake Terry Baker amesema nyota huyo hawezi kumshukuru kwa kusema hivyo lakini anahitaji msaada wa haraka ili kumuepusha na kadhia hiyo. Baker amesema wakati alipomuona katika mipindi kabla ya sherehe za Noel Novemba mwaka jana alikuwa yuko sawa lakini hivi sasa hali hiyo imebadilika na anadhani hata mwenyewe Gazza analijua hilo. Naye golikipa nyota wa zamani wa klabu ya Manchester United, Peter Schmeichel alikitaka Chama cha Wachezaji wa Kulipwa kuingilia kati suala hilo na kuangalia jinsi ya kumsaidia nyota huyo ambaye amewahi kucheza katika vilabu vya Newcastle United, Tottenham Hotspurs, Lazio na Rangers.

AL BADRY ASIKITIKA KUONDOKEWA NA NYOTA WAKE KADHAA.

MENEJA wa klabu ya Al Ahly ya Misri, Hossam Al Badry amebainisha kuwa alitaka kuachana na timu hiyo wiki iliyopita baada ya bodi ya klabu hiyo kuwauza kwa mkopo baadhi ya wachezaji wake nyota. Klabu hiyo iliwapeleka wa mkopo mshambuliaji nyota wa klabu hiyo Mohammed Abo Trika katika klabu ya Baniyas ya Muungano wa Falme za Kiarabu-UAE pamoja na Ahmed Fathi na Mohammed Nagy Gedo katika klabu ya Hull City ya Uingereza. Al Badry amedai kuwa alitaka kuondoka mara tu nyota hao walipoondoka lakini hivi ameelewa kuwa ni kutokana na matatizo ya kifedha yanayoikabili klabu hiyo ndio maana bodi ikaamua kufanya hivyo. Kocha amesema anafikiri ataendelea kuwepo klabuni hapo ingawa hata hivyo amesikitishwa kuondokewa na nyota wake hao.

OBI MIKEL MCHEZAJI WA MWAKA WA GOAL.COM NIGERIA.

KIUNGO nyota wa kimataifa wa Nigeria na klabu ya Chelsea John Obi Mikel amekubali tuzo ya mchezaji bora wa mwaka kwa mashabiki wa Nigeria waliopiga kura katika mtandao wa Goal.com. Asilimia 36.84 ya wasomaji wa mtandao huo nchini Nigeria walimpigia kura Obi Mikel ambaye alikuwa akipambanishwa na mchezaji mwenzake wa Chelsea Victor Moses huku wengine wakiwa ni Ahmed Musa, Kano Pillars na Rueben Gabriel wote wanacheza CSKA Moscow ya Urusi na John Utaka wa klabu ya Montpellier ya Ufaransa. Akipokea tuzo hiyo kutoka kwa Mhariri Mtendaji wa mtandao wa Goal.com nchini Nigeria Lalade Adewuyi, Obi Mikel aliwashukuru mashabiki na kueleza nia yake ya kuingoza nchi hiyo kunyakuwa taji la michuano ya Mataifa ya Afrika pamoja na nchi yao kutopewa nafasi hiyo. Nigeria ambayo itakwaana na Ivory Coast katika mchezo wa robo fainali ya Afcon baadae leo huku wadau wengi wa soka wakiipigia chapuo Ivory Coast iliyosheheni wachezaji nyota wanaong’ara kwenye vilabu mbalimbali barani Ulaya kusonga mbele katika mchezo huo.

BAO LA KUJIFUNGA LA RONALDO LAIZAMISHA MADRID.

MSHAMBULIAJI nyota wa klabu ya Real Madrid, Cristiano Ronaldo jana alifunga bao lake la kwanza la kujifunga na kuipa ushindi wa bao 1-0 Granada hivyo kufifisha matumaini yao kidogo ya kutetea taji la Ligi Kuu nchini Hispania maarufu kama La Liga. Ronaldo ambaye ameifungia Madrid mabao 21 katika ligi msimu huu, alijifunga bao hilo dakika ya 22 ya mchezo huo wakati akijaribu kuokoa mpira kona uliopigwa kuelekea katika lango lao. Matokeo hayo yanaifanya Madrid kutofautiana na vinara wa La Liga Barcelona kwa alama 15 ambao wanaweza kuongeza pengo hilo kufikia alama 18 kama wakishinda mchezo wao wa leo dhidi ya Valencia. Madrid mpaka sasa wamejikusanyia alama 43 katika michezo 22 ya ligi waliyocheza na kubakia nyuma ya Atletico Madrid wanaoshika nafasi ya pili kwa tofauti alama nne ambao wataikaribisha Real Betis baadaye leo.

NCHI ZA AFRIKA MAGHARIBI ZATAWALA AFCON.

MICHUANO ya Mataifa ya Afrika-Afcon inayoendelea nchini Afrika Kusini imeonekana kutawaliwa na nchi za Afrika Magharibi baada ya kuingiza timu saba katika hatua ya robo fainali. Hii ni mara ya kwanza kwa upande mmoja kuingiza timu nyingi katika hatua hiyo toka robo fainali ilipoanza rasmi mwaka 1972 baada ya kupanuka kwa mashindano hayo kufikia timu 12. Nchi saba hizo kutoka Afrika Magharibi zilizofuzu hatua hiyo ni pamoja na Cape Verde waliokuwa kundi A, Ghana na Mali waliofuzu kupitia kundi B, Burkina Faso na Nigeria kundi C na Ivory Coast na Togo kundi D. Nchi pekee ambayo haipo katika Muungano wa Soka kwa Nchi za Afrika Magharibi-WAFU na ilifaulu kufika hatua ya robo fainali ni wenyeji Afrika Kusini. Hata hivyo wenyeji hao nao wametolewa kwenye mchezo wa robo fainali uliofanyika jana kwa changamoto ya mikwaju ya penati na Ghana hivyo kubakisha nchi za upande huo pekee zikitamba kugombea taji hilo la Afcon.

C.Ronaldo Own Goal Granada Vs Real Madrid 1-0 HD 2/2/2013