MSHAMBULIAJI nyota wa kimataifa wa Brazil, Neymar jana ametua katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Oliver Tambo uliopo jijini Johannesburg akiongoza kundi la wachezaji wan chi hiyo wanaocheza soka Ulaya tayari kwa ajili ya mchezo dhidi ya Bafana Bafana utakaochezwa kesho katika Uwanja wa FNB. Neymar alikuwa ameongozana na nyota wengine ambao ni Thiago Silva, Dante, Daniel Alves na Marcelo huku wengine wakiwemo viungo Fernandinho, Paulinho, Bernard na Hulk likiwa fungu la mwisho la wachezaji wanaocheza Ulaya kuwasili. Mashabiki walimiminika katika uwanja huo pamoja na hali ya manyunyu yaliyokuwa yakidondoka kwa ajili ya kumona nyota huyo wa Barcelona huku mmoja wao akifanikiwa kusogea karibu na kupiga picha naye kabla hajapanda katika basi lililokuwa likiwasubiri. Brazil ambayo inanolewa na kocha Luis Felipe Scolari inatarajiw akufanya mazoezi yao ya mwisho leo kabla ya mchezo huo.

Tuesday, March 4, 2014
HALI YA KISIASA UKRAINE YALETA SINTOFAHAMU YA MECHI YA KIRAFIKI DHIDI YA MAREKANI.
RAIS wa Shirikisho la Soka nchini Ukraine Anatoliy Konkov amesema wachezaji wa timu ya taifa ya nchi hiyo hawatasafiri kwenda Cyprus kwa ajili ya mchezo wa kirafiki wa kimataifa dhidi ya Marekani utakaochezwa kesho lakini Chama Cha Soka cha Marekani kinaamini mchezo huo utakachezwa kama ulivyopangwa. Mchezo huo mara ya kwanza ulitakiwa kuchezwa jijini Kharkiv lakini ulihamishwa na kupelekwa Cyprus kwasababu ya matatizo ya kisiasa na baada ya Marekani kuomba hivyo. Konkov amesema kwasasa hawawezi kucheza mashindano ya kitaifa kwasababu hawaruhusiwi kucheza katika ardhi yao ya nyumbani hivyo haoni umuhimu wa kwenda Cyprus katika kipindi hiki ambacho nchi yao iko katika matatizo. Rais huyo aliendelea kudai kuwa wanacheza soka kwa ajili ya watu wao na nchi yao hivyo timu yao haitasafiri kwenda Cyprus badala yake itabakia nyumbani. Wakati Konkov akitoa kauli hiyo Shirikisho la Soka la Marekani liliandika katika mtandao wake wa twitter kuwa mechi hiyo itachezwa kama ilivyopangwa kwakuwa shirikisho la Ukraine lilithibitisha timu yao kusafiri kwenda Cyprus. Mvutano huo umekuja kufuatia rais wa Urusi Vladimir Putin kupata kibali kutika katika bunge la nchi hiyo kutumia nguvu za kijeshi dhidi ya Ukraine katika rasi ya Crimea hatua ambayo inapingwa na Marekani na mataifa mengine barani Ulaya.
PALIOS ASHANGAZWA NA KAULI YA CAMPBELL.
OFISA mkuu wa zamani wa Chama cha Soka nchini Uingereza-FA, Mark Palios amesema ameshangazwa na kauli ya Sol Campbel aliyedai kuwa hakuchaguliwa kuwa nahodha wa timu ya taifa ya Uingereza kwasababu ya rangi yake. Campbell mwenye umri wa miaka 39 anaamini kuwa angeweza kuwa nahodha wa nchi hiyo kwa miaka 10 kama angekuwa mweupe. Akihojiwa Campbell ambaye ameichezea Uingereza mechi 73 amesema anadhani FA walikuwa wakitamani awe mzungu. Palios ambaye aliiongoza FA mwaka 2003-2004 amesema kauli hiyo imemshangaza kwasababu sio jukumu la FA kuteua manahodha wa timu ya taifa bali jukumu hilo analo kocha. Campbell ambaye amewahi kuwa beki wa Arsenal na Tottenham huku akiichezea Uingereza kuanzia mwaka 1996 hadi 2007 aliwahi kuwa nahodha wan chi hiyo mara tatu wakati timu ikiwa chini ya Sven Goran Eriksson.
BARCELONA INAWEZA KUSHINDA MATAJI MATATU MSIMU HUU - FABREGAS.
KIUNGO mahiri wa klabu ya Barcelona, Cesc Fabregas amedai kuwa hana shaka kwamba wanaweza kunyakuwa mataji matatu msimu huu. Barcelona kwasasa inashika nafasi ya pili katika msimamo wa La Liga wakiwa nyuma ya mahasimu wao Real Madrid kwa alama moja huku wakikaribia kujihakikishia nafasi ya kutinga robo fainali ya Ligi ya Mabingwa kwa kuongoza kwa mabao 2-0 dhidi ya Manchester City na pia wakiwa wametinga fainali ya Kombe la Mfalme. Fabregas anakubali kuwa Barcelona bado haijafika katika kiwango chake cha juu lakini ana uhakika kuwa msimu huu unaweza kuwa na mafanikio kwao. Nyota huyo wa kimataifa wa Hispania amesema bado wanatakiwa kukuza kiwnago chao cha uchezaji lakini kila kitu bado kiko ndani ya uwezo wao kwasababu bado wamebakiwa na mechi 19 mbele yao za ligi, Ligi ya Mabingwa na Kombe la Mfalme na kama wakifanikiwa kushinda zote utakuwa msimu mzuri kwao.
CARDIFF CITY MATATANI BAADA YA TAJIRI WAKE KUTOA OFA YA JANGUSHO.
LIGI Kuu nchini Uingereza inatarajia kuichunguza klabu ya Cardiff City baada ya mmiliki wake Vincent Tan kuahidi kutoa bakshishi ya paundi milioni 3.7 kwa wachezaji wake kabla ya mchezo waliofungwa na Tottenham Hotspurs Jumapili. Kwa mujibu wa sheria za ligi hiyo kila timu inapaswa kuwasilisha taratibu za kutoa bakshishi zao kabla ya kuanza kwa msimu hivyo Tan tayari amevinja sheria hiyo kwa kutoa bakshishi hiyo ili kuzuia timu yake isishuke daraja. Kwa mujibu wa mtandao wa Sportsmail tajiri huyo hakutoa bakshishi yoyote kwa kikosi cha Cardiff ili kuzuia isishuke daraja kabla ya msimu kuanza kwasababu hakuamini kama wanaweza kuwepo katika nafasi hiyo hivi sasa. Badala yake Tan alifanya ziara ya kuitembelea timu hiyo katika hoteli waliyofikia ya Hilton Jumamosi usiku na kutoa ofa hiyo kwa wachezaji ingawa hata hivyo haikusaidia sana kwani waliambulia kipigo.
UAFRIKA UNAMUANGUSHA YAYA TOURE - NASRI.
MSHAMBULIAJI wa klabu ya Manchester City, Samir Nasri amedai kuwa Yaya Toure angeheshimika zaidi kama angekuwa sio Mwafrika. Wachezaji walifunga mabao maridani ambayo yaliisaidia City kutoka nyuma na kuifunga Sunderland kwa mabao 3-1 na kufanikiwa kunyakuwa Kombe la Ligi. Lakini wakati akiulizwa ubora wa mchezaji mwenzake huyo, kiungo huyo wa kimataifa wa Ufaransa alidai kuwa kutokana na ukweli kwamba Toure anatoka Ivory Coast hiyo inamfanya asipate heshima yake anayostahili. Nasri amesema kama Toure angekuwa sio Mwafrika kila mtu angesema ndio kiungo bora duniani kwasababu anaweza kufanya kila kitu, kufunga, kuzuia na kushambulia. Nyota huyo aliendelea kudai kuwa ni tofauti kwasababu anatokea Ivory Coast lakini kama angekuwa anatoka Argentina au Brazil kila mtu angekuwa na mzungumzia na wangeweza kulipa hata paundi milioni 40 au 50 kwa ajili yake.
KESI YA PISTORIUS YAENDELEA KUNGURUMA.
MAWAKILI wa mwanariadha nyota wa Afrika Kusini Oscar Pistorius wameanza tena kumhoji shahidi muhimu. Kesi ya Pistorius ilianza hapo jana katika makahama iliyopo jijini Pretoria. Jana shahidi mmoja wa upande wa waendesha mashtaka, Michelle Burger ambaye ni jirani wa Pistorius aliieleza mahakama kuwa alisikia kile alichokitaja kama kelele za mauaji zikitoka katika nyumba anayoishi Pistorius, zilizofuatiwa na milio ya bunduki, katika usiku ule alipomuua mpenzi wake. Mwanariadha huyo wa paralimpikic ambaye miguu yake imekatwa na hukimbia kwa kusaidiwa na miguu bandia amekana mashitaka na kudai kuwa alimpiga risasi mpenzi wake Reeva Steenkamp bila kukusudia baada ya kudhania kuwa alikuwa ni mtu alievamia nyumba yake.
Subscribe to:
Posts (Atom)